Samia arudisha mikopo ya asilimia 10

Ni kusaidia vijana walioacha 'unga'

RAIS Samia Suluhu Hassan ameagiza asilimia 10 ya fedha za halmashauri kwaajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na walemavu alizozisitisha Machi mwaka huu zirejeshwe tena ili kuwasaidia vijana hususani waliopona kutokana na uraibu wa dawa za kulevya, kuweza kujiajiri.

Pia alionya wamiliki wa gereji za magari kutokana na baadhi ya wafanyakazi wao kuchukua unga wa moshi ulio kwenye exosi za magari na kuwauzia vijana hao ambao huuchanganya na dawa za kulevya na kuvuta au kujidunga.

Samia alibainisha hayo wakati akifunga maadhimisho ya kupiga vita dawa za kulevya duniani ambayo kitaifa yalifanyika jijini Arusha jana.

Maadhimisho hayo yalibeba kaulimbiu isemayo: ‘Zingati utu, boresha huduma za kinga na tiba’.

Rais Samia alitoa maagizo hayo baada ya vijana hao waliokuwa wanajihusisha na matumizi ya dawa za kulevya kumweleza kuwa baada ya kupona wamekuwa hawana kazi ya kufanya, hivyo wakaomba serikali iwasaidie kupata mikopo ya kufanya biashara.

Vijana hao walioomba msaada kwa Rais Samia ni pamoja na Grace Mbarawa aliyekuwa anatumia dawa za kulevya aina ya heroini kwa miaka 10, Habibu Mohammed aliyekuwa akitumia heroini kwa miaka 15, Judith James aliyetumia heroini kwa miaka 13 na Twaha Mtunga.

“Zile fedha tulizozisitisha za halmashauri, ile asilimia 10, mmewasikia hapa wanalalamika kwamba tukishapona hatuna cha kufanya, sasa hii asilimia 10 Waziri Mkuu atakaa na Tamisemi na wengine wanaohusika kuzielekeza halmashauri kuja na mpango mzuri kama ni kupitia benki au vyovyote, lakini vijana hawa waunganishwe na halmashauri wafikie ile asilimia 10 hasa ile asilimia nne ya vijana kama ni wanaume na kama ni wanawake ni asilimia nne ya wanawake wapate ili wafanye kile wanachotaka kufanya,”alisema.

Pia aliitaka Wizara ya Afya, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, asasi za kiraia, Tamisemi na wadau wa maendeleo kushirikiana ili kuhakikisha vijana hao wanapata afua zitakazowafanya wasirudie tena uraibu wa dawa za kulevya na badala yake wajikite kwenye kazi za uzalishaji.

Rais Samia Suluhu Hassan akisikiliza maelezo kutoka kwa mmoja wa wataalamu wanaoshiriki maonesho ya Maadhimisho ya kitaifa ya kupiga vita matumizi na biashara ya dawa za kulevya duniani yaliyofanyika kitaifa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha jana. Wa pili kulia ni Waziri Mkuu. Kassim Majaliwa. (Picha na Ikulu)

Rais Samia alisitisha fedha hizo za halmashauri Machi 29 mwaka huu wakati akipokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na kubainisha kuwa kuna upotevu mkubwa wa fedha katika halmashauri kutokana na mifumo hususani wa kutumia mashine ya POS.

Aidha, alisema Tanzania imefanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa zaidi ya asilimia 90 huku akiwataka watendaji wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kutobambikiza watu kesi za dawa za kulevya.

Alisema ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya dawa za kulevya na uhalifu (UNODC) inaonesha kuwa Tanzania imefanikiwa kupunguza uingizaji wa dawa za kulevya kwa zaidi ya asilimia 90.

Pia alisema Tanzania imekuwa kinara kwenye kudhibiti kemikali bashirifu jambo lililoifanya UNODC kupitia Bodi ya Kimataifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya (INCD) kutambua kazi hiyo na kuipa Tanzania heshima ya kutoa mafunzo ya udhibiti wa kemikali hiyo katika nchi tisa ikiwemo Burundi, Rwanda, Zambia, Madagascar, Ethiopia, Malawi, Eritrea, Msumbiji na Mauritius.

Pia aliwataka watendaji wa mamlaka hiyo kuzingatia weledi na uadilifu katika kazi zao na wasikubali kutumika kubambikia watu kesi kwa kuwakomoa bali wazingatie maslahi ya nchi na kutenda haki.

Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo pamoja na mambo mengine alisema mafanikio waliyoyapata kwa miaka sita tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo mwaka 2017 ni kushinda mashauri ya dawa za kulevya 987 kati ya mashauri 1,648 yaliyotolewa uamuzi ambao jumla ya mashauri yote yaliyofanyiwa kazi kwa hatua mbalimbali ni 6,818.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x