Samia: Asante Kamala, karibu tena

RAIS Samia Suluhu Hassan amemshukuru Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris kwa ziara ya kihistoria ya kuitembelea Tanzania, akisema itasaidia kuimarisha uhusiano wa mataifa hayo mawili. Rais Samia ameyasema hayo katika ukurasa wake wa Twitter akimuaga kiongozi huyo wa juu wa Marekani baada ya kuhitimisha ziara ya siku tatu nchini.

Alisema utekelezaji wa mambo waliyojadili utasaidia kusukuma mbele zaidi uhusiano wa mataifa hayo. “Ahsante Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris kwa safari yako ya kihistoria Tanzania, utekelezaji tuliyojadiliana vitasukuma uhusiano wa Tanzania na Marekani kwenda mbele zaidi kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Safari njema na karibu tena Tanzania,” ameandika Rais Samia ambaye kama Kamala, ana historia ya kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kushika wadhifa wa juu.

Kamala alikuwapo nchini tangu juzi kwa ziara kwa mwaliko wa Rais Samia, juzi baada ya mazungumzo yao, waliwaeleza waandishi wa habari makubaliano kadhaa ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi zao mbili. Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewaongoza Watanzania kumuaga Makamu huyo wa Rais wa Marekani katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Kamala aliondoka jana saa 5:30 asubuhi akiongozana na mumewe, Douglas Emhoff baada ya ziara iliyokuwa na manufaa kwa Watanzania kwa kusaini makubaliano kadhaa ya kuisaidia katika nyanja mbalimbali.

Akiwa JNIA, Kamala na mumewe waliangalia ngoma za utamaduni wa Kitanzania kabla ya kuagana na wenyeji wake na kupanda ndege yao ya C-32 Air Force II na kuondoka kwenda nchini Zambia kuhitimisha ziara yake ya siku tisa barani Afrika.

Ulinzi na usalama ulikuwa wa hali ya juu huku wakishuhudiwa maofisa wa usalama wa Marekani wakiwa juu ya majengo ya Terminal I na wengine wakiranda wakifanya doria kwa kutumia mbwa na farasi. Dk Mpango alikuwa wa kwanza kuwasili kiwanjani hapo saa 5:10 asubuhi kisha robo saa baadaye saa 5:25 msafara wa Harris uliwasili na taratibu za kuondoka kuanza.

Miongoni mwa walioongozana na Dk Mpango kumuaga Kamala ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji, Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Dk Elsie Kanza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla.

Kamala aliwasili Machi 29, mwaka huu saa 5:05 usiku akitokea Ghana ikiwa ni ziara ya siku tisa katika mataifa matatu barani Afrika; Ghana, Tanzania na Zambia. Miongoni mwa mambo aliyofanya akiwa nchini ni kuzungumza na Rais Samia ambako walikubaliana masuala kadhaa ambayo ni pamoja na kukubali kuisaidia nchi katika kukabiliana na virusi vya Marburg. Mbali na hilo, Kamala aliahidi pia kushirikiana na Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kusaidia katika vita dhidi ya ugaidi. Aidha, alitembelea Makumbusho ya Taifa na kuweka shada la maua katika Mnara wa Kumbukumbu ya waliopoteza maisha katika shambulio la kigaidi mwaka 1998 kwenye Ubalozi wa Marekani nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button