RAIS Samia Suluhu Hassan amesema yeye si mtu wa maneno mengi bali ni vitendo zaidi na hata watu wakisema yeye anasonga mbele kuhakikisha maendeleo ya Watanzania yanapatikana.
Kauli hiyo aliitoa eneo la Tengeru aliposimama kuwasalimia wananchi akiwa njiani kuelekea Arusha katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya kupiga vita dawa za kulevya yanayofanyika leo katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini humo.
“Mimi sina maneno mengi, vitendo ndio vingi, wakisema mimi nafanya masikio hivi, naangalia wapi nakwenda kwa hiyo waseme, sisi tunafanya, tunajenga kesho kwa ajili ya vijana, serikali yenu iko makini na tuko ‘sober’ tunajipanga vyema kuwatumikia wananchi,” alisema Rais Samia.
Alisema mambo mengi yanakwenda vizuri mfano ni sekta ya elimu, umeme, afya, maji na kusema maeneo hayo serikali imejitahidi na bado itaendelea kuyaboresha ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Kuna mambo tunapaswa kufanya, lakini umeme, elimu, maji, tumejitahidi, vijana wa vyuo mmesikia bajeti ya mwaka huu, tumejitahidi kupunguza gharama hasa kwa wanaoingia vyuo vya kati,” alisema Rais Samia.
Alisema serikali itaendelea kuboresha sekta nyingine kama kilimo, biashara na sasa inajipanga vizuri kutoa huduma kwa vijana wa Kitanzania ili wasipoteze muda wazalishe mali na kuustawisha uchumi wa nchi na familia zao.
“Serikali bado ina mipango mikubwa ya kuwatumikia, tunatafuta njia za kuifungua nchi kukaribisha sekta binafsi, tufanye nao kazi maeneo tofauti tofauti na hii yote ni kutengeneza ajira kwa vijana wetu na kukusanya fedha zaidi ili tutoe huduma zaidi kwa Watanzania,” alisema Rais Samia.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa soko la kisasa la Tengeru, Rais Samia alisema hiyo ni ahadi ya serikali na bado iko palepale.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella alimshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa huo.
Awali, Mongella akizingumzia kampeni ya kupambana na matumizi ya dawa za kulevya mkoani humo, alisema mkoa huo umefanya kampeni kabambe ya kuelimisha umma kuhusu madhara ya dawa za kulevya na wananchi wameelewa na hata wale waliokuwa wakilima bangi nao wameelimishwa ili kuachana nacho.
Alisema kuna wakati jamii haikushirikishwa wala kuwa na elimu na baada ya kuelimishwa wametambua na sasa kila mmoja ni mlinzi wa mwenzake katika kupiga vita dawa hizo.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Emmanuela Kaganda alisema wameamua kupiga vita dawa za kulevya ikiwemo kilimo cha bangi na wanatekeleza kwa njia tofauti na awali.
“Tumekuja na njia tofauti kidogo, awali tuliwakimbiza wakulima wa bangi na kuwanyang’anya bangi, sasa tunafanya njia shirikishi ya kukaa na wahusika na kujifunza kwa nini wameingia kwenye kilimo cha bangi na tumewaelimisha na kuwapa mazao mbadala ya kulima kuachana na bangi,” alisema Kaganda.
Alisema eneo la Arumeru ni zuri kwa sababu lina rutuba nyingi na hivyo baadhi ya wakulima waliamua kulima bangi bila kujua madhara yake na baada ya elimu wametambua na sasa wanalima mazao ya chakula na biashara na kuachana na bangi.
Mapema mwezi huu, Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo alisema maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Vita Dawa za Kulevya Duniani ina lengo la kuongeza uelewa katika jamii na kuhamasisha umma kuachana na matumizi ya dawa hizo.
“Tumelenga kuongeza uelewa kwa jamii na kuhamasisha umma kushiriki katika mapambano dhidi ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya, maadhimisho haya yataambatana na maonesho ya shughuli mbalimbali za udhibiti zinazofanywa na mamlaka pamoja na wadau wake,” alisema Lyimo.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ni: “Tuzingatie Utu na Kuboresha Huduma za Kinga na Tiba”.
Imeandaliwa na Ikunda Erick, Dar na Veronica Mheta, Arusha