RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa Mahakama kuwa na macho makali kwenye ngazi za chini za mahakama kwa sababu ni eneo ambalo mambo mengi ya hovyo yanaendelea na kusababisha wananchi wakose haki.
Rais Samia alisema hayo jana katika hafla ya kuwaapisha viongozi wateule wakiwamo majaji wa Mahakama ya Rufaa na Mwenyekiti wa Baraza la Maadili iliyofanyika katika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.
Alisema kuna mashaka makubwa yanayotokana na utendaji wa mahakama katika ngazi za chini, kwa kueleza kuwa kuna kila dalili za rushwa, na alitoa mfano wa sakata la hivi karibuni la wafugaji mkoani Lindi waliofanya makosa kwa kuingiza mifugo mahali pasipostahili.
Rais Samia alisema katika kesi hiyo, wafugaji walifanya makosa ya waziwazi na kukamatwa kwenye makosa, na jaji aliamua kwenda hukohuko kujionea makosa hayo, lakini cha kustaajabisha alirudi na kukanusha kuwa wafugaji hao hawana makosa.
“Tumesikia kesi ya Lindi, ambapo wafugaji wamekamatwa kwenye makosa jaji akasema nami nakwenda hukohuko kutizama, na kurudi akasema hawana makosa, sasa utajiuliza kuna nini hapo?” Alihoji Rais Samia. Aliongeza kuwa kuna kesi nyingi kwenye hifadhi za Tanzania kama Tanapa (Shirika la Hifadhi za Taifa), lakini zikifika mahakamani “mambo magumu kidogo wafugaji ile pesa wanaifanyia kazi kwelikweli.”
Akiwageukia majaji wanaoboronga, Rais Samia alisema ni vema wanaoondolewa kwa kuboronga watajwe wakati wakiondolewa na sio kufichaficha. “Stara iko kubwa huko kwenu mnawastiri, hamtaki waadhirike…tungependa kujua nani kaondolewa kwa bahati mbaya,” aliongeza Rais Samia.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliwapongeza majaji hao na kuwaambia Watanzania wana mategemeo makubwa ya kupata haki kutokana na utendaji wao, na kuongeza kuwa mhimili wa serikali hauna mashaka kwa kuwa historia na utendaji wao vinaongea.
Aliongeza kuwa viongozi hao wana uadilifu mkubwa na uzoefu wa utoaji wa haki na katika kuwasaidia Watanzania kufahamu namna ya kupata haki, serikali ilizindua programu ya kuwasaidia wananchi kufahamu haki zao.
Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson mbali na kumpongeza Rais Samia kwa kufanya uteuzi uliozingatia usawa wa kijinsia, kama mwakilishi wa wananchi, anatamani hukumu za mahakama zitoke kwa haraka ili wananchi wapate haki. Aliongeza kuwa ingawa haki iliyoharakishwa ni sawa na haki iliyofukiwa, pia haki iliyocheleweshwa ni sawa na haki aliyonyimwa mtu.
“Katika kuyatazama hayo yote ninyi mnaenda katika mahakama ya juu katika nchi yetu na tunawategemea sana,” aliongeza Dk Tulia ambaye kitaaluma ni mwanasheria. Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alimshukuru Rais Samia kwa kutekeleza jambo la kihistoria katika Mahakama kwa kuongeza idadi ya majaji kutoka majaji wa rufani 25 hadi 31 baada ya kuapisha majaji sita.
Profesa Juma alisema kuwa na idadi kubwa ya majaji wa rufani ni faida kwa Mahakama kwa kuwa itaimarisha utendaji pamoja na kuongeza vikao vya majaji wa rufani kwa sababu kazi ya Mahakama ya Rufani inafanyika kwa vikao. Alisema Mahakama ya Rufaa sasa itakuwa na uwezo wa kukaa na kufanya vikao tisa kutoka vikao saba kutokana na idadi ya majaji wa rufani waliopo kwani kila kikao kinahitaji majaji watatu, watano mpaka majaji saba.
“Kwa wastani hadi Aprili 30, mwaka huu kulikuwa kuna mashauri 5,636 ambayo yalikuwa yamesajiliwa Mahakama ya Rufani na ukiyagawa katika haya majopo na kila jopo lina uwezo wa kushughulikia mashauri 33 pekee, hivyo kwa majaji sita mzigo ulikuwa 805, lakini baada ya kuwapata majaji sita mzigo utashuka hadi 626,” alisema Profesa Juma.
Majaji walioapishwa jana kuwa majaji wa Mahakama ya Rufaa ni Jaji Zainab Muruke, Jaji Leila Mgonya, Jaji Amour Said Khamis, Jaji Dk Benhaji Masoud, Jaji Gerson Mdemu, Jaji Agnes Mgeyekwa pamoja na Jaji mstaafu Rose Teemba ambaye ameapishwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maadili.