Samia asifu uungwana wa Membe

Samia asifu uungwana wa Membe

RAIS Samia Suluhu Hassan ameongoza mamia ya waomboleaji kuaga mwili wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe (69).

Membe aliagwa Dar es Salaam jana na anatarajiwa kuzikwa kesho kijijini kwake Rondo alipozaliwa kilichopo mkoani Lindi.

Rais Samia alisema kiongozi huyo alikuwa muungwana, mchapakazi na aliipenda nchi yake na watu wake.

Advertisement

“Kifo cha Membo kimewasikitisha wengi, ndani na nje ya nchi, aliwagusa wengi, alikuwa muungwana sana,” alisema na kuongeza:

“Membe aliipenda nchi na watu wake, alipenda pia mataifa mengine na tumesikia alishiriki kuleta amani katika mataifa ya nje, amefanya kazi katika kulinda utu na heshima ya mtu,mchango wake mwingi kwa taifa na mataifa mengine umeshasemwa, tuzidi kuomba Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi Amina,”

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax alisema Membe alikuwa kiongozi mahiri aliyehuduma serikalini na alikuza diplomasia.

“Alifanya kazi kwa weledi na ameacha alama kwenye mioyo ya viongozi wengi, mchango wake utaendelea kubaki historia njema, utumishi wake ulitukuta alikuwa miongoni mwa viongozi waliochangia kuwepo kwa sera ya mambo ya nje,” alisema Dk Tax.

Alisema Membe alikuwa kiongozi aliyependa kuwatia moyo na ujasiri wengine na anakumbuka yeye ndiye aliyemtia ujasiri wakati ameteuliwa kwenda kuwania nafasi ya uongozi ndani ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC).

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo alisema ni nadra kuwapata watu kama Membe.

“Chama tumepokea kwa mshtuko taarifa za kifo chake, maisha yake ya uongozi ndani ya chama na serikali yana mengi sana, alitenda haki na hakuwa mchoyo wa maarifa alitengeneza vijana wengi ikiwemo Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye ni wazi chama kimepoteza mtu muhimu sana” alisema Chongolo.

Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe alisema Membe alikuwa kiongozi aliyesimamia haki, ukweli na demokrasia na katika kumuenzi anawakumbusha wanadamu waishi kama Mungu anavyotaka.

“Membe ametufundisha, tuishi kama Mungu anavyotaka, tusimamie haki,ukweli na demokrasia,tukemee maovu na kuyazuia kama Mungu anavyoelekeza,” alisema Zitto.

Kiongozi wa mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, Balozi wa Comoro, Dk Ahamada El Badaoui Mohamed alisema msiba huo umewashtua na unahuzunisha.

Membe alifariki dunia Mei 12 mwaka huu katika Hospitali ya Kairuki alikopelekwa alfajiri ya siku hiyo baada ya kusikia maumivu kifuani na kukohoa.

Aligundulika kuwa na tatizo kwenye mapafu lililomsababishia kifo chake muda mfupi baadaye. Ameacha mke, Dorcas Masanche na watoto watatu, Cecilia, Richard na Denis.

Membe alizaliwa mwaka 1953 kijijini Rondo, Lindi akiwa mtoto wa pili kati ya watoto saba wa familia ya mzee Kamillius Ntachile.

Alipata elimu ya msingi kati ya mwaka 1962-1968 mkoani Lindi, elimu ya sekondari, 1969-1972 katika Seminari ya Namupa, Lindi na mwaka 1973-1974 alihitimu kidato cha sita katika Seminari ya Itaga, Tabora.

Alisoma shahada ya kwanza katika Sayansi ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 1981-1984, mwaka 1990 -1992 alisoma shahada ya umahiri katika uchumi na uhusiano wa kimataifa UDSM.

Pia alijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na mafunzo mengine yakiwemo ya siasa katika Chuo cha Kivukoni wakati huo ameshajiunga kulitumikia taifa serikalini na ndani ya CCM na aliendelea kushika wadhifa hadi nafasi ya uwaziri na baadaye kugombea nafasi ya urais.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *