SERIKALI imelieleza Bunge kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kinara wa utawala bora nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hayo bungeni Dodoma jana wakati akihitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Simbachawene alisema Rais Samia hana ubaguzi kwa misingi ya vyama, dini, ukabila wala ukanda na ameamua kujenga nchi moja yenye mshikamano hivyo aungwe mkono.
Hoja hiyo ya Simbachawene ilikuja baada ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani (CHADEMA) kulieleza Bunge kuwa baadhi ya watumishi wa umma kwenye Wilaya ya Nkasi wamepigwa marufuku wasimpe ushirikiano kwa jambo lolote.
Kutokana na hilo, Simbachawene alimhakikishia Khenani kuwa atalifanyia kazi jambo hilo kwa kuwa Rais Samia hana ubaguzi kwa mtu yeyote.
Katika hoja hiyo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angellah Kairuki kulifuatilia jambo hilo na atapata taarifa kutoka kwa Khenani.
Pia Dk Tulia alimtaka Khenani na Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema) kumpelekea ushahidi wa madai yao kuwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) katika maeneo yao, unawahudumia wananchi kwa msingi ya ubaguzi wa kisiasa.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete alisema kuhusu Tasaf kuna maeneo likiwamo la utambuzi wa wanufaika halina budi kufanyiwa maboresho ili wahusika wanufaike na mfuko huo.
Kuhusu madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wa umma, alisema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita, jumla ya Sh bilioni 2.4 zimeshalipwa na serikali itahakikisha inamaliza malimbikizo madeni yote yaliyobaki.
Kwa kuwa wastaafu wengi husumbuka kupata mafao yao, Dk Tulia alimuagiza Simbachawene kuhakikisha katika mwaka ujao wa fedha tatizo la wastaafu kusumbuka kupata mafao yao linakwisha kwa kuwa watu hao kisheria hutoa taarifa miezi sita kabla ya kustaafu.
Alisema bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha wa 2023/24 ni ya kuimarisha mifumo ya serikali ikiwemo inayowahusu watumishi wa umma.
Simbachawene aliwaeleza wabunge kuwa kuna mifumo mipya iliyojengwa zaidi ya 15 ambayo itasaidia katika masuala ya udhibiti na mifumo mingi iliyoanzishwa haijaanza kutumiwa kwa asilimia 100.
“Ipo mifumo ambayo itatusaidia katika kusimamia utendaji kazi wa watumishi, ipo mifumo itakayotusaidia kujua mtumishi mmoja mmoja yupo wapi na anafanya nini, ipo mifumo ambayo itatusaidia ulipaji wa mishahara na taarifa za kila mtumishi.
“Leo tu Mheshimiwa Spika nimebonyeza nikajua tuna upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi 11,336,” alisema Simbachawene.
Alisema moja ya misingi ya utawala bora ni uwazi, hivyo hakuna watakachoficha na watapeleka mifumo ambayo hawajaimalizia kwa majaribio ili wabunge waone uhalisia.