Samia ataka elimu ujuzi vyuo vikuu
RAIS Samia Suluhu Hassan amevitaka vyuo vya elimu ya juu na taasisi za elimu kuhakikisha elimu wanayotoa kwa wanafunzi wao ni ya ujuzi na maarifa ya kukidhi mahitaji ya soko ili waitumie kuleta tija na maendeleo.
Alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana aliposhiriki Mahafali ya 52 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambako pia alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari na Mkuu wa chuo, Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Katika mahafali hayo, wahitimu 2,115 walitunukiwa shahada wakiwamo 141 wa Shahada ya Uzamivu (PhD), Shahada ya Uzamili, Shahada ya Awali, Stashahada na Astashahada.
Rais Samia alisema elimu inabadilika hivyo lazima vyuo viendane nayo ili kupata wahitimu wenye ujuzi na maarifa yanayokubalika katika maisha ya sasa.
“Elimu inayotolewa na taasisi zetu za elimu ya juu na vyuo lazima iwe toshelevu, wahitimu watoke na ujuzi na maarifa ambayo watayatumia kuleta tija na maendeleo na waendane na mahitaji ya soko la sasa na baadaye,” alisema Rais Samia. Alisema amefurahi UDSM imeanza kupitia mitaala yake ili kuona kama inaendana na mahitaji ya soko na dunia ya sasa.
Aliagiza vyuo vingine vya elimu viige mfano huo ili kuwa na mitaala inayotoa ujuzi na kuwajengea maarifa wahitimu. “Niwahakikishie vyuo vyote kuwa serikali itatoa ushirikiano wa kutosha pale inapohitajika na tutaendelea kuongeza bajeti lengo ni kutomuacha mtu nyuma,” alisema.
Aliwaasa wahitimu kuwa dunia inawasubiri hivyo ni vyema waende kutumia ujuzi na maarifa waliyopata kuwa vitendo ili maendeleo yakaonekane kupitia wao. Awali, Mwenyekiti wa Baraza la UDSM, Balozi Mwanaidi Sinare alisema baraza hilo liko macho kuhakikisha sera na miongozo inayopitishwa inafanyiwa kazi kwa kuzingatia malengo ya chuo.
Alisema baraza limekuwa likifuatilia kwa karibu masuala ya kitaaluma ikiwamo udahili na usajili wa wanafunzi, mitihani, uanzishwaji na mapitio ya programu mbalimbali ili kuhakikisha ubora na vigezo vya kitaaluma vinazingatiwa.
Alisema baraza hilo limeidhinisha sera na mapendekezo mbalimbali ikiwemo sera ya umataifishaji ya chuo hicho ili kuhakikisha uamuzi wowote kuhusu mitaala, ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na maendeleo ya chuo yanaendana na Dira ya UDSM ya mwaka 2061.
“Katika dhana ya chuo kuwa na hadhi ya kimataifa na ikizingatiwa mazingira ya elimu ya juu yanazidi kubadilika kwa kasi chuo hakiwezi kubaki nyuma. Hata hivyo, tuna wajibu wa kujipanga kimkakati kuvutia watafiti wa kimataifa na kutayarisha kizazi kijacho cha wahitimu na wasomi ambao wanapaswa kufikia viwango vya kimataifa na kukubalika na kuheshimiwa duniani,” alisema Balozi Sinare.
Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye aliwataka wahitimu hao wawe wepesi kutafuta fursa badala ya kusubiri ziwafuate. Profesa Anangisye alisema endapo ajira serikalini na sekta binafsi itachelewa wahitimu hao wawe wepesi kuzitafuta sehemu nyingine ambako watatumia maarifa na ujuzi wao kwa ufanisi zaidi.
“Mnaenda kujiunga na jamii kama sehemu ya nguvukazi muhimu, mfahamu kuwa mnaingia katika ulimwengu unaobadilika haraka, ni muhimu na nyie mkawe wepesi wa kujifunza mambo mapya na kubadilika kwa haraka ili msiachwe nyuma ya wakati,” alisema.
Aliongeza: “Naomba mkumbuke mnakwenda kuingia katika ulimwengu unaobadilika haraka ni muhimu mkawe wepesi wa kujifunza mambo mapya na kubadilika kwa haraka ili msiachwe nyuma na wakati.”