Samia ataka kongamano la vijana kuhusu maadili
RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka waandaaji wa Kongamano la Wanawake wa Kiislam Zanzibar katika maadhimisho ya Mwaka Mpya wa Kiislamu 1445 – Hijiria, kuandaa kongamano linalohusu vijana kwa kuwa ndio walengwa wakuu katika mmomonyoko wa maadili.
Ameyasema hayo leo Julai 16, katika kongamano la wanawake wa Kiislamu lililofanyika Zanzibar na kusema kuwa vijana ndio walengwa wakubwa.
Pia amewataka wanawake kujielimisha vizuri na kuwa na elimu ya aina zote kidini na kidunia, ili waweze kuwa walimu wazuri na kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.
“Tanzania inashuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili, unyanyasaji wa kijinsia na wizi na matumizi ya dawa za kulevya.
Mambo haya yanaua kizazi, na chanzo chake kikubwa ni kukosekana kwa misingi mizuri ya elimu ya dini.
“Bila kutafuna maneno niseme sote tunashuhudia mmonyoko wa maadili nchini na tunakubaliana kuwa ni ugonjwa unaotuandama.
“Jamii yetu inaathirika sana na masuala ya udhalilishaji wa kijinsia, wizi, dawa za kulevya na mengineyo ambayo sisi kama wazazi na walezi au wakuu wa familia zetu yanatutia aibu sana, yanatudhalilisha, yanatuondolea heshima na haiba nchini kwetu, na pia nadiriki kusema yanatuulia vizazi vyetu.
“Lakini tumeyaacha yamekuwa mpaka hapa tulipofikia leo. Ukiangalia kiundani kwa nini tumefika hapa leo, ni ukosefu wa elimu ya msingi ya dini, tungekaa wote tukajua dini inasema nini vijana wetu wote wakaelemishwa dini inasema nini, imani za kidini, makatazo ya kidini tusingefikia hapa.
“Naona hapa kuna wanawake wakurugenzi, mainjinia, wabunge, wake wa viongozi ambao kwa namna moja au nyingine wamefanya vitu vikubwa katika jamii, lakini bado kuna changamoto kubwa ya maadili, wanawake tunakwama wapi? Amehoji na kuongeza:
“Naomba tukae tujitafakari, katika ulimwengu wa leo ambao wanawake wapo mstari wa mbele kupigania haki, kushiriki mambo ya kitaifa, kijamii kufanya kazi ambayo huko nyuma ilionekana si kazi za mwanamke, lakini leo tunazifanya tena kwa uadilifu na weledi mkubwa.”
“Wakina mama mnavyokaa majumbani na mashoga zenu, mnasengenya wenzenu Watoto wanashuhudia wanapita, wakirudi wanasikia anajidai kunywa maji kumbe anataka kusikia kinachosemwa.
-“Lakini pia wakishuhudia wakisutana, kuzodoana, kuzushiana ni sisi tutakaa tuzushe jambo huna ushaidi unalizungumza kwa fahari, watoto wanasikia, wanasoma nini?
Hawawezi kuchukua mazuri watachukua mabaya, kwa hiyo tufanye yaliyo mema ili watoto waige,” amesema.