Samia ataka uchunguzi fedha za ‘plea bargain’
RAIS Samia Suluhu Hassan ameonesha kushangazwa na fedha zilizokusanywa za adhabu ya makubaliano baada ya kukiri kosa (plea bargain), ambazo zimepelekwa kwenye akaunti China na kutaka Tume ya kuangalia jinsi ya kuboresha taasisi za haki jinai nchini kuchunguza suala hilo kwa kina.
Rais Samia ameyasema hayo leo Januari 31, 2022 Ikulu Chamwino mjini Dodoma, akizindua tume hiyo ambayo inaongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othman Chande, ambayo itakuwa na jukumu kubwa la kufanya maboresho ya haki jinai ili kukidhi matakwa ya serikali na jamii ya Tanzania kwa ujumla.
Taasisi za haki jinai zitakazofanyiwa kazi na tume hiyo ni Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Jeshi la Magereza, na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Rais Samia, amesema ofisi ya Mashtaka (DDP), ni kiini kinachotengeneza kesi katika mlolongo wa kutafuta haki, na kutaka paangaliwe kwa kina kuna kasoro zipi? Nini kimetokea.
“Nakumbuka nyuma kidogo, Tume ya Taifa ya Mashtaka kulikuwa kuna ngoma kubwa kidogo inachezwa mpaka kukusanya fedha za wale wa plea bargain, fedha za plea bargain nyingine zimeonekana na nyingine hazijaonekana, uki-trace utaambiwa kuna akaunti China sijui imepeleka pesa zipi, tukatazame haya yote, ofisi ya mashtaka kuna nini,” amesisitiza Rais Samia.
Rais Samia amesema kuwa mfumo wa haki jinai nchini umevurugika, sababu ya kupuuza sio kwa kuwa hakuna mifumo ya maadili, ipo ila inapuuzwa, katika kila taasisi zilizotajwa zina mifumo yake ya maadili ila kuendana nayo ndio imekuwa tatizo.
“Kutokana na hayo na kupokwa kwa haki hasa kwa wasio na mamlaka wala fedha, na wale waliokuwa wanafanya makosa wanaepushwa na makosa kwa sababu ya fedha zao na mamlaka yao.
“Nimeona tupitie upya mifumo yetu tumekosea wapi tuboreshe wapi ili twende vizuri, sasa nimeamua kuunda tume hii nikitambua mmetoka katika taasisi hizo zinazoenda kuchunguzwa, mfano Takukuru, Dk Hosea ulikuwepo humo naamini utatusaidia, Ma IGP mpo wawili mlikuwepo humu, ‘ethics; mnazijua mlikosea wapi mnajua.
“AG mmetoka huko mhimili wa mahakama mnaijua huko kipi kiboreshwa, rushwa iliyokithiri kwa sasa naona imepungua hata hivyo mifumo ya kazi iboreshwe, mifumo isomane, hakuna jaji ataweza kuchenga chenga,”amesema.
Rais Samia pia amelinyooshea kidole Jeshi la Polisi na kudai kuwa mara nyingi ukizungumza na watu 100 basi watu 70 watanyoosha kidole kwa jeshi la polisi.
“Takukuru na yenyewe kuna nini humo ndani watu wanazuia au wanahamasisha rushwa humo ndani kupo kusafi kiasi gani, kubadilisha wakuu wa taasisi haisaidii akiingia anakuta tayari kuna mizizi lazima utamshinda tu,” amesema.