MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan ameagiza wanawake wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wawe na uthubutu katika siasa na uchumi.
Alisema hayo Dodoma jana wakati akifungua Mkutano wa 10 wa (UWT) ambao pamoja na mambo mengine, umefanya Uchaguzi Mkuu wa jumuiya hiyo.
“Wanawake wengi wetu tunajifungia, tunauendekeza uanamke hata tukiwa kwenye vikao…ukiwa na mawazo unashindwa kuzungumza unaogopa kukosolewa au kulaumiwa na usiposema unarudisha taasisi nyuma. Ni uthubutu pekee unaweza kuifanya taasisi isonge mbele sio unajua kitu unashindwa kusema unaogopa kulaumiwa unaogopa kunyimwa kura,” alisema Rais Samia.
Alisema wanawake wana nafasi ya kufanya mambo makubwa hivyo kinachotakiwa ni uthubutu na kufikiri zaidi ya yale wanayowaza. Rais Samia aliiagiza UWT itekeleze miradi mikubwa ili kuongeza nguvu za kiuchumi.
“Wito wangu mwende kufanya miradi mikubwa ambayo itaipa jumuiya nguvu ya kiuchumi…kama mnavyojua uwezo wa kiuchumi ndio unanunua uwezo wa kisiasa, tusiposimama vizuri na kutokuwa na nguvu ya kiuchumi huenda tukanunuliwa kisiasa,” alibainisha.
Aidha, Rais Samia aliagiza UWT wapambane na vitendo vya udhalilishaji hasa kwa watoto.
“Suala ambalo UWT hatujalifanyia kazi vizuri ni udhalilishaji na sio kwetu sisi tuliokubuhu bali udhalilishaji kwa watoto, na idadi ya kesi za udhalilishaji kwa watoto zimekuwa zikiongezeka hapa nchini, hivyo ni vyema UWT kusimama kidete kupambana na tatizo hili,” alisema Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Aidha, aliiagiza UWT itafsiri kwa vitendo Mpango wa Tatu wa Maendeleo uliolenga kujenga uchumi shindani. Alisema serikali imejenga miundombinu ya barabara, reli, usafiri wa angani na majini na upatikanaji wa maji na umeme.
Kuhusu janga la njaa, alisema serikali imejiandaa kulikabili kwa kuongeza bajeti ya kilimo mara tatu, kuweka miundombinu ya umwagiliaji, upatikanaji wa pembejeo na kujenga maghala ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula.
Mwenyekiti wa UWT anayemaliza muda wake, Gaudentia Kabaka alisema asilimia 99 ya uchaguzi katika ngazi za kata, wilaya na mikoa zimefanyika vizuri.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana aliwataka wanawake kushikamana wakati wote na kuwa nguvu ya chama ni umoja na mshikamano ndani ya chama. Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo aliwataka viongozi na wanachama wa UWT kuweka mbele maslahi ya chama badala ya mtu.
Wakati huohuo, katika uchaguzi huo mbunge wa zamani wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda alishinda uenyekiti wa UWT Taifa baada ya kuwabwaga aliyekuwa akitetea nafasi hiyo, Kabaka na Katibu Mkuu wa zamani wa UWT, Kate Kamba.
Chatanda alipata kura 527, Kabaka kura 219 na Kate Kamba kura 8.