Samia atangaza neema Mchuchuma, Liganga

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mradi wa kuchimba chuma Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma itaongeza fursa za ajira na mapato ya halmashauri hivyo wananchi washirikinena na serikali kuutekeleza.
Alisema hayo jana alipozungumza kwa simu na wananchi wa Njombe wakati viongozi wa serikali walipokwenda kuzindua mchakato wa kulipa fidia wananchi wanaopisha miradi hiyo.
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji na Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthoy Mtaka walikuwa miongoni wa viongozi hao.
“Mchuchuma na Liganga sasa inakwenda kuchangamka, ajira zinakwenda kupatikana, kodi kwa halmashauri inakwenda kupatikana kutokana na mradi kuwepo kwa hiyo niwaombe wananchi tushirikiane katika utekelezaji”alisema Rais Samia.
Aliongeza”Tushirikiane katika malipo, kila mtu achukue anachostahiki halafu kwa vema kabisa tuje tushikiane kwenye mtekelezaji wa mradi”
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Dk Nicholaus Shombe alisema hadi jana wananchi 36 walikuwa wamelipwa fidia hiyo na wote wanaostahili watalipwa kupisha miradi hiyo.
Serikali inalipa fidia ya Sh bilioni 15.4 wananchi kwa ajili ya kupisha uchimbaji wa chuma cha Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma wilayani Ludewa mkoani Njombe.
Juzi Dk Kijaji alilieza HabariLEO kuwa utaratibu wa kulipa fidia ni kwamba kila mwananchi anayehusika atawekewe fedha zake kwenye akaunti yake ya benki.
Alisema wananchi takribani 1,042 watalipwa fidia hiyo kwa kuwa serikali imeshaipatia wizara hiyo fedha kwa ajili ya kulipa fidia hiyo.
“Kwa kuwa serikali imeshatupatia fedha zote shilingi bilioni 15.4, kwa hiyo tumeanza kulipa kuanzia leo (juzi), siku ya leo (juzi) tu tumeshalipa shilingi bilioni tano kwenye akaunti za wananchi,”alisema Dk Kijaji
Wakati akiwasilisha bungeni Dodoma makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 alisema kuanzia Oktoba hadi Desemba mwaka jana walifanya uhakiki wa mali za wananchi wanaopisha mradi wa makaa ya mawe Mchuchuma katika vitongoji vya Nkomang’ombe, Idusi, Kilomos, Ntiule na Mhambalasi.
Dk Kijaji alisema kati ya wananchi 651 waliotakiwa kuhakiki taarifa zao, wananchi 580 walijitokeza, sawa na asilimia 87.
Alisema kuanzia Oktoba – Desemba mwaka jana wizara hiyo ilifanya uhakiki katika eneo la Liganga katika vitongoji vya Mnyusi, Ilongi na Myorua katika Kijiji cha Mundindi na Kitongoji cha Luhaha katika Kijiji cha Amani
Dk Kijaji alisema kati ya waathirika 494 waliotakiwa kuhakiki taarifa zao, 481 walijitokeza sawa na asilimia 98.
Alisema Aprili mwaka huu wizara ilipokea shilingi bilioni 15.4 kwa ajili ya ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha miradi ya Liganga na Mchuchuma.