Samia atoa maagizo manne Magereza

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo manne kwa Jeshi la Magereza Tanzania ikiwemo kuzingatia weledi, kuzingatia haki zote kwa wafungwa, kuboresha utawala bora na kuhakikisha wanarekebisha tabia za wafungwa.

Rais Samia alisema hayo wakati akiwaapisha majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Kamishna Jenerali wa Magereza, Mzee Ramadhani Nyamka, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Alisema taasisi ya Magereza imeaminiwa kulinda maisha na haki za watu waliowekwa ndani na akasema wafungwa wana haki zao.

“Nakutaka uongoze taasisi hii kwa weledi mkubwa. Taasisi hii iliacha njia ya ile kazi ya msingi ya kurekebisha tabia za hawa watu na kulinda haki zao. Hawa ni wanadamu kama wengine, wanatakiwa kupata hewa safi, mavazi na chakula kizuri. Sio kwamba mhalifu basi na adhabu ziwe nyingi kumweka kule tu ni adhabu. Kalinde haki zao,” aliagiza.

Rais Samia aliagiza jeshi hilo lirejee katika wajibu wake pia wa kurekebisha tabia za wafungwa ili watu waache kufanya makosa.

“Tunatoa misamaha ya wafungwa lakini mtu anasamehewa leo baada ya siku mbili karudi akiulizwa anasema sasa nifanyeje huku nje? Anarudi jela akijua atakula ugali na kupata mahali pa kulala. Lakini mngerekebisha akaujua ubaya wa kuwa kule na akitoka afanye nini asingetaka arudi tena,” alisema.

Aidha, alisema Magereza pia inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo utawala bora ambao hauko sawa na kumtaka Kamishna huyo wa Magereza kurekebisha changamoto hiyo ikiwemo kuwapeleka watu kwenye mafunzo.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni utawala wenye kusimamia haki za wale wanaotumikia taasisi hiyo na kufanyakazi ya msingi kurekebisha tabia za wafungwa.

“Si wote wanaokuja huko ni wahalifu wamekubuhu, wengine wanafanya kwa bahati mbaya, wengine hawakufanya na wengine ni ushahidi wa mazingira, hata nyie mnajua ndio maana mmetenga magereza. Nataka mkafanye urekebishaji wa tabia,” alisema.

Kuhusu matumizi ya fedha, Rais Samia alisema moja ya makosa ya jeshi hilo ni kutofuata sheria kwenye matumizi ya fedha.

Alisema katika bajeti ya mwaka huu, 2022/23 jeshi hilo limeongezewa bajeti na kuagiza fedha hizo ziende kwenye magereza yote kutoa huduma kwa wafungwa hao.

Awali, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alizungumzia suala la umuhimu wa kutenganisha shughuli za magereza na biashara na kumhakikishia Rais kuwa watasimamia maelekezo yote aliyoyatoa.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button