Samia atoa maagizo mifumo TRA, bandari

RAIS Samia Suluhu Hassan amekerwa kwa mifumo ya bandari na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutosomana.

Akizungumza leo Machi 29, 2023  mara baada ya kupokea ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Salum Hamduni, Rais Samia amesema kitendo cha mifumo ya hizo taasisi mbili kutosomana ni makusudi ili watu wapate upenyo wa kupiga pesa.

“Bandari na TRA hawasomani wakati Bandari ndiyo pointi kubwa ambako TRA wanakusanya fedha, sasa mifumo isiposomana, hii ni makusudi ili watu waweze kuchomoa pesa. Kuna tatizo gani la kufanya TRA na bandari mifumo isisomane? Hakuna.

“Kwa hiyo nawataka TRA na Bandari wakae kitako wahakikishe mifumo inasomana. Nimeambiwa TRA sasa kuna Wakorea wapatao wengi tu wamekuja kwa sababu ya mifumo, Waziri wa Fedha (Mwigulu Nchemba) Wakorea wasiondoke mpaka tuhakikishe mifumo hii inasomana,” amesema Rais Samia.

Amesema hakuna mtu yeyote kutoka sekta binafsi atakubali kuingiza fedha wakati mifumo haisomani.

“Muhimu mifumo ya bandari, teknolojia iboreshwe, private sekta iingie, bandari inaweza kuchangia nusu ya pesa ya bajeti yetu, bandari private sekta ikaribishwe ili bandari iimarishwe.

“Mifumo ya Bandari na TRA ingekuwa inasomana tungefanya wonders, na hakika kama tutaweka vizuri mifumo, tutaweka ‘private’ sekta tutakusanya pesa ya kutosha tuna kasoro ya makusanyo asilimia 3.8 kwa hiyo bado tuna kazi kubwa ya kufanya,”amesema.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button