Samia atoa maelekezo matumizi ya mtandao serikalini

RAIS Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo matano kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha mifumo ya tehama inayotumika ndani ya wizara na taasisi za serikali zinasona.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Agosti 10, 2023 katika uzinduzi wa Mkongo wa Mawasiliano wa Baharini (Submarine Cable) wa 2 Afrika na Teknolojia ya Mawasiliano ya Kasi ya 5G ya Airtel Mbezi Bechi Tanki Bovu jijini Dar es Salaam

Amesema, alishatoa maelekezo mara mbili, na leo mara ya tatu anarudia tena anataka maelekezo hayo yafanyiwe kazi kwa haraka.

“Nilishasema mara mbili, hii mara ya tatu natarajia kuona utekelezaji.”Amesema Rais Samia na kuongeza
“Wizara na taasisi zote zinazotoa huduma kwa watanzania hususani mabenki, Wizara ya elimu, afya, na wizara nyingine zote ebu sasa twendeni tukatumie namba moja tu ya mtanzania anapoambiwa Samia namba 20 ndani ya Tanzania basi taasisi zote zikivuta namba 20 awe Samia mmoja yule yule, taarifa zile zile;…. “maana sasa hivi naweza kuwa namba 20 NIDA, nikienda benki kuna taarifa nyingine, afya taarifa nyingine, shule taarifa nyingine, hii inaleta shida hata kwenye usalama wa nchi, tunataka kujua nani ni nani.

“Mwenyeji wa Tanzania ajulikane, mgeni ajulikane, itatupunguzia, ninapotaka huduma mahali ile lete hiki, lete kile, lete barua ya mtendaji, nikitoka hapo naenda taasisi nyingine lete lete lete, hii itatupunguzia lete lete.

“Sasa tunakazi ya kukagua taarifa za watu wote waliopo kwenye NIDA, kwa hiyo kila Mtanzania ahakikishe taarifa alizotoa NIDA ni sahihi kama kuna taarifa hazipo sawa akazirekebishe ili tuweze kutambuana nani ni nani ndani ya nchi yetu.

“Itarahisisha pia kwa upande wa NIDA, namba wanazotoa kwa watanzania akizaliwa tu leo akipewa cheti cha hospitali ‘automatic’ anapata namba na taarifa zake zinaanza kukusanywa kuanzia pale, alizaliwa hospitali gani, kilo ngapi, ana afya hana, Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) simamia hilo.” Ameagiza Rais Samia.

Pia, agizo la pili Rais Samia ametaka Wizara hiyo ya Habari inayoshughulika pia na masuala ya tehama kuhakikisha kufanya tathmini ya gharama ambazo zitatumika kuunganisha taasisi za serikali.

“Agizo la pili kwa mujibu wa takwimu za TCRA za Machi mwaka huu, jumla laini za simu za mkononi na mezani zilikuwa 61,879,725 simu za mkononi zilikuwa 61, 795, 208 kati ya hizo asilimia 73 ni simu zinazotumia 2G asilimia 27 ni vifaa kama vishikwambi, kompyuta mpakato na simu zinazotumia 3G, 4G na 5G ambapo simu janja ni asilimia 22 na vifaa vingine ni asilimia 5.

“Sasa hapa nitoe wito Waziri Mkuu, Wizara ya Tehama, na E Government, serikali kwetu bado hatujajipanga vizuri, matumzi ya mtandao bado hatujayatumia vizuri naomba tujipange tufanye tathmini tunahitaji kiasi gani kuziunganisha wizara na taasisi za serikali kutumia mitandao.

“Kama ni mafunzo kwa watendaji wapewe serikali iende kwenye mtandao, tukifanya hivyo tutanusuru mambo mengi kwanza taarifa kupotea, ufanisi ndani ya taasisi za serikali utaongezeka kwa sababu ni kujibizana kwa kutumia mtandao.

Rais Samia amesema kuwa jana alipokea ripoti kutoka moja ya kamati alizoziteua ambapo katika taarifa yake ilidai kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa kwa sababu ya mawasilino duni.

“Kamati hiyo imeniambia kulikuwa na ucheleweshaji mwingi kwa sababu mawasiliano yanaingia kwa email kutoka nje, kuna mtu anaigeuza email kuwa karatasi, karatasi iwekwe kwenye folda ipelekwe kwa mkubwa, mkubwa ndio aione haishushe chini, kama mkubwa hayupo imechelewa.

“Lakini kama kungekuwa na kusomana email inapokuja unaweka komenti unaishusha kwa mwingine, mwingine anashusha kwa amwingien kazi imekwisha kwa simu moja maofisini bado tuna ‘traditional method’ za kufanya kazi haiwezekani.”Amesema

Agizo la tatu alilotoa Rais Samia ni Wizara ya Habari , Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), iharakishe mchakato wa matokeo ya stadi zitakazotoa mwelekeo wa bei za sms, data na simu kwa kipindi cha 2023 mpaka 2027.

“Matokeo ya stadi yatatupa dira kamili ili tuone stadi inasemaje, maendeleo ya kwenda 5G yanasemaje ili tujue njia gani tunapita kutoa huduma kwa watanzania,”amesema.

Aidha, agizo la nne alilotoa Rais Samia ni kuitaka Wizara hiyo ya Habari inayohusika na Tehama kuweka mkakati wa kuweka huduma ya WiFi bure kwenye maeneo muhimu ikiwemo vyuoni na kwa wafanyabiashara wadogo maarufu ‘Machinga’.

“Vyuoni huduma za WiFi ipelekwe kwa haraka ili wanachuo wapate mtandao kwa haraka wasome vizuri na wakamilishe masomo yao viuzri, maeneo ya biashara machinga na wenzao kule nako wanahitaji, ila wito wangu kwa machinga kutumia mitandao vizuri sio kusengenya, kupeleka uzushi, kuzushi usio na maana, kutumia mitandao hii kwa faida zao wenyewe na wala sio faida ya serikali.

Aidha, agizo la tano Rais Samia ameitaka Wizara na taasisi husika kuhakikisha zinafuatilia ahadi ya Airtel kujenga madarasa 100 ya kisasa na kuweka WiFi za bure kufuatiliwa kwa karibu na ahadi hizo zikamilike.

Habari Zifananazo

Back to top button