Samia atoa pole kifo cha mtoto wa mzee Mwinyi

RAIS Samia Suluhu Hassan amempa pole Rais mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kwa kufiwa na mwanawe, Hassan Ali Hassan Mwinyi (70).

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia alieleza kusikitishwa na kifo hicho.

Hassan ni kaka wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi.

“Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Hassan Ali Hassan Mwinyi, mtoto wa Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi na kaka wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi. Nawapa pole wanafamilia kwa msiba huu. Mwenyezi Mungu amrehemu Hassan na amjaalie Pepo. Inna lillahi wa inna ilayhi rajiuun,” aliandika Rais Samia jana.

Mamia ya wananchi wakiwemo viongozi wakuu wa serikali walihudhuria mazishi ya Hassan kijijini kwao Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hassan aliwahi kuwa mtumishi mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na serikali ya Muungano akiwa na nyadhifa mbalimbali.

Aliaga dunia katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kuugua kwa muda mrefu.

Mazishi hayo yalihudhuriwa na viongozi wakiongozwa na Rais mstaafu Mwinyi, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, marais wastaafu wa Zanzibar akiwemo Dk Aman Abeid Karume, Dk Ali Mohamed Shein na Waziri mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

Wakati huohuo Rais Samia alieleza kupokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Rais wa zamani wa Urusi, Mikhail Gorbachev.

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x