WADAU wa masuala ya sheria wameunga mkono agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwamba polisi wamalize upelelezi kwanza kabla ya kumweka mtu mahabusu.
Rais Samia amemuagiza Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai kuhakikisha unafanyika upelelezi na kuwa na ushahidi wa kutosha kabla ya kumweka mtuhumiwa mahabusu.
Alitoa agizo hilo Jumanne Moshi mkoani Kilimanjaro wakati anafungua kikao kazi cha maofisa waandamizi wa Jeshi la Polisi Makao makuu na makamanda wa mikoa na vikosi.
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Dk Edward Hoseah alisema mtu hastahili kupelekwa mahakamani kama upelelezi haujakamilika.
Dk Hoseah alisema madhara ya kumpeleka mtu mahakamani kabla ya upelelezi kukamilika ni pamoja na kumuumiza kwa kumharibia heshima yake na kuifanya familia yake kuishi kwa wasiwasi wakati wote.
Pia alisema mahakama inaweza kutupilia mbali kesi hiyo au Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) anaweza kuachana na kesi hiyo.
“Alilosema Mheshimiwa Rais ni sahihi, hata wakati wa kampeni zangu mwaka juzi nilikuwa nikilisema hili kwamba usimpeleke mtu mahakamani kabla hujakamilisha upelelezi, huu ndiyo msimamo wangu na ndiyo msimamo wa sheria,” alisema Dk Hoseah.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile alisema polisi hawapaswi kumkamata mtu kabla hawajakamilisha upelelezi, bali watafute kwanza ushahidi wa kujitosheleza ili mtu anapokamatwa apelekwe moja kwa moja mahakamani.
“Mtu anaathirika zaidi kisaikolojia hasa kwa yule ambaye hajatenda hilo kosa, hata kama anatoka nje kwa dhamana, lakini bado ni mtuhumiwa na jamii inajua kuwa ni mtuhumiwa,” alisema Mwambipile.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema kinachofanyika nchini ni kinyume kwa kuwa inatakiwa upelelezi ukamilike kwanza ndipo mtu akamatwe.
Henga alisema kama hakuna ushahidi mtu hapaswi kukamatwa na ndicho kitu alichosisitiza Rais Samia.
“Kitu kinachotakiwa kufanyika ni kurekebisha Sheria ya Makosa ya Jinai kwa sababu ina mapengo ikiwemo suala la upelelezi kwanza haisemi, pia ina mapengo kwenye makosa yasiyo na dhamana na yenye dhamana,” alisema Henga.
Alisema madhara ya upelelezi kuchelewa ni makubwa kwa kuwa haki iliyocheleweshwa ni haki iliyonyimwa kwa kuwa kama mtu alitakiwa asikilizwe ndani ya siku 10 akasikilizwa ndani ya siku 100, anapata mateso kutokana na uzembe wa kutosikilizwa.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto kupitia katika mtandao wa kijamii wa twitter alimshukuru Rais Samia na kusema kuwa hivi ndivyo inavyopaswa kuwa mtu asikamatwe bila ushahidi kukamilika.
Zitto alisema kauli hiyo ilete mabadiliko ya mfumo wa haki jinai ikiwamo kwa kila kosa kuwa na dhamana isipokuwa baadhi tu ukiwemo uhaini.
Wakili wa Kujitegemea, Daniel Kalasha alisema kwa kuwa jinai ya zamani na sasa ni tofauti kutokana na uhalifu mwingi kutekelezwa kwa kutumia teknolojia, serikali hainabudi kuwekeza kwenye teknolojia ili ithibitishe pasipo shaka.
“Kama serikali haijawekeza vizuri kwenye namna ya kufanya upelelezi kwa kutumia teknolojia, bado tutakuwa na safari ndefu,” alisema Kalasha.
Aliongeza: “Kwa mfano Zanzibar wamefunga karibu mji mzima CCTV kamera, ina maana kama kuna kosa la jinai linafanyika, serikali inakwenda kwenye CCTV itakupata tu kwa urahisi badala ya kutumia mfumo wa zamani wa kumtafuta mtu.”
Alisema teknolojia inawasaidia wapelelezi kufanya kazi yao kwa urahisi na mahakama kutenda haki kwa urahisi.
Alisema makosa ya jinai hayana ukomo kwa mujibu wa sheria kama ilivyo kwa mashauri ya madai na kwenye jinai kama mtu amekosa cha kuthibitisha kesi inakuwa imekufa.