Samia avipongeza vyombo vya habari kwa kazi nzuri

Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan amevipongeza vyombo vya habari nchini kutokana na kufanya kazi nzuri mwaka jana kwa kuandika habari ambazo hazikuligawa taifa wala kuleta chuki nchini.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema Dodoma jana kuwa Rais Samia ametuma salamu hizo za pongezi kwa vyombo vya habari kwa kazi nzuri hiyo.

“Rais Samia anavishukuru vyombo vya habari kwa kazi nzuri katika mwaka 2022 ya kuandika habari za kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha na kubwa kuliko yote ni kuunganisha taifa,” alisema Nape wakati anazungumza na waandishi wa habari.

Advertisement

Rais Samia anawashukuru wanahabari na vyombo vya habari kwa kushirikiana naye kwa mwaka mzima kwa kufanya kazi kubwa hiyo ya kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha umma bila kuandika habari za kutenganisha taifa.

Nape alisema Rais Samia amevishukuru vyombo kwa kuandika habari nzuri katika mwaka mzima kama taifa halikushuhudia habari za kuligawa wala kuleta chuki bali za kuunganisha taifa.

“Hatujashuhudia habari za kugawa taifa na kuleta chuki,” alisema.

Rais amekuja na falsafa ya 4R au R4 ya kuridhiana, ustahimilivu, mabadiliko na kujenga upya na vyombo vya habari vimeunga mkono dhana hiyo na wameanza kujadili vizuri dhana hiyo.

Kutokana na kuandika habari nzuri taifa limesonga mbele na kufikia hapa tulipo. Hatujashuhudia habari zinazoligawa taifa.

Wakati huohuo serikali imeunda kamati ya watu tisa kutathmini hali ya uchumi wa waandishi katika vyombo vya habari nchini na imepewa miezi mitatu kukamilisha kazi hiyo.

Nape alisema kamati hiyo itaongozwa na Mwenyekiti Tido Mhando ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni za Habari za Azam.

Katibu wa Kamati hiyo atakuwa Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa na wajumbe ni Mkurugenzi Mtendaji kampuni ya habari ya Mwananchi (MCL), Bakari Machumu, Mkurugenzi Mtendaji ITV na Redio One, Joyce Mhavile, Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (Tamwa), Dk Rose Reuben.

Wajumbe wengine ni Mkurugenzi Mtendaji Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Kenneth Simbaya, Mkuu wa Maudhui Clouds Media Group, Sebastian Maganga, Mkurugenzi Mtendaji Multichoice Tanzania, Jacqueline Waiso na Mwandishi wa Habari, Richard Mwaikenda.

Nape alisema kamati hiyo itafanya kazi ya kuchakata taarifa ya hali ya uchumi wa waandishi wa habari, kupata taarifa ya hali ya waandishi wa vyombo walioajiriwa, wenye mikataba, wasioajiriwa, wawakilishi mkoani na wengine wakilishi, hali za ajira za waandishi na vipato vyao, kipato chao na mikataba yao.

Kamati hiyo pia itaangalia utaratibu wa mikataba na hali ya mikataba iliyosainiwa kama yaliyomo yanaheshimiwa, walichokubaliana mwandishi katika mkataba ndicho kinalingana na maslahi yanalingana na hali halisi.

Pia watafanya tathmini ya sababu ya changamoto zinazotokea na njia ya kuzikabili na utapendekezwa ufumbuzi kwenye vyombo vya habari vyenyewe na serikalini.