DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan amevunja Bodi ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pia amemteua Mkurugenzi mpya wa Shirika la Bima la Taifa.
Taarifa ya Ikulu Mawasiliano iliyotolewa leo Novemba 9,2023 inasema kuwa Rais Samia amevunja bodi hiyo ya TCRA tangu juzi Novemba 7, 2023.
Bodi hiyo ilikuwa ikiongozwa na Mhandisi Othman Sharif Khatib ambae alikua Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti ni Khalfan Saleh na wajumbe ni Dk Mzee Suleiman Mndewa, Fatuma Simba, Ikuja Abdallah, Batenga Katunzi na Rehema Jessica Khalid.
Aidha, taarifa hiyo inasema kuwa Rais Samia amemteua Kaimu Abdi Mkeyenge kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC).
Kabla ya uteuzi huo, Mkeyenge alikua Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Meli Tanzania (TASAC), anachukua nafasi ya Dk Elirehema Doriye ambae anapangiwa majukumu mengine.
Pia, Rais Samia amemteua Balozi Said Hussein Massoro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kuwait, akichukua nafasi ya Balozi Said Shahib Musa ambae ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu kuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Awali, Massoro alikua Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) nafasi aliyoteuliwa January 3, 2023 akichukua nafasi ya Athuman Diwani.
Hata hivyo nafasi hiyo alidumu kwa kwa siku 238 tu ambapo Agosti 28 mwaka huu Rais Samia alimteua kuwa Balozi na nafasi yake kuchukuliwa na Balozi Ali Idi Siwa.
Aidha, amemteua Balozi James Gilawa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini akichukua nafasi ya Balozi Meja Jenerali Gaudence Milanzi ambae amestaafu.