RAIS Samia Suluhu Hassan amewaagiza majaji wafanye kazi kwa kuzingatia haki, weledi na maadili.
Alisema hayo jana katika Ikulu ya Chamwino Dodoma baada ya kuwaapisha majaji na Kamishna Jenerali wa Magereza.
Rais Samia alisema uapisho huo wa majaji 21 kati ya 22 umejaza idadi ya majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani.
“Nitaendelea kufanya uteuzi kwa jinsi Katiba inavyoelekeza na hali ya uchumi itakavyokuwa,” alisema.
Rais Samia aliwataka majaji wafanye kazi kwa wananchi kwa kuwa njia ya majaji hao ni haki.
“Mungu aliwapangia muwe majaji. Lakini pia tunajua mtenda haki pekee ni Mungu lakini alipendezewa uwepo kwenye huo mhimili wa kutoa haki. “Ukifanya vinginevyo unamkosea Mungu wako aliyetaka uwe hapo. Nawaombeni kafanyeni haki na si vingine,” alisema.
Rais Samia alisema hajawahi kukataa maombi ya mahakama zikiwemo safari na mafunzo na anafanya hivyo ili wakabadilishane mawazo na uzoefu na wenzao.
“Kama ni mbinu mpya basi mnajifunza mbinu mpya ndio maana sijawahi kuzuia. Lengo langu ni mkajifunze mhimili wa Mahakama usimame, ili muachane yaliyokuwa yakisemwa huko nyuma. Mahakama huko nyuma hazikuwa vizuri lakini kwa sasa angalau husikii sana malalamiko ya wananchi,” alisema.
Aliongeza: “Nawataka mkafanye kazi kwa uadilifu, weledi na unyenyekevu mkubwa. Kama mlivyosema katika kiapo chenu, nawatakia heri na fanaka katika kazi zenu.”
Awali, Rais Samia alisema tangu aingie madarakani Machi mwaka jana ikiwa ni miezi 17 sasa ameteua majaji 43 wa Mahakama Kuu na tisa Mahakama ya Rufani wakiwemo wanawake 23 na 27 wanaume.
Alisema malalamiko ya wananchi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mhimili wa mahakama yamepungua na akasifu weledi wa majaji wanawake.
“Wanakuwa weledi sana, wanahukumu kwa moyo kama ni mtoto anamuangalia mtoto kama mama pamoja na kufuata sheria anaangalia mila, desturi na tamaduni za Tanzania,” alisema Rais Samia.
Alisema hateui wanawake kwa sababu ni wanawake ila anapima sifa na uwezo wao ikiwemo kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Mahakama na kuwasisitiza wanawake wasimuangushe.
Awali Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango alihimiza majaji wafanye kazi kwa kuzingatia haki.
“Mmepewa dhamana kubwa na Watanzania wana imani kwamba mtatimiza wajibu na viapo vyenu mlivyoapa mbele ya Rais na Watanzania. Kabla sijaja hapa nilijiuliza Jaji ni nani, Kamusi ya Kiswahili toleo la tatu la Bakita linasema jaji ni mtu mwenye taaluma na dhamana ya kusimamia, kusikiliza kesi na kutoa hukumu kwa mashtaka mahakamani,” alisema Dk Mpango.
Alisema hata katika vitabu vya dini vimebainisha wazi kuwa majaji hawatakiwi watende yasiyo ya haki katika hukumu, wasipendelee mtu masikini wala kumstahi mwenye nguvu bali wahukumu jirani kwa haki.
“Neno haki mkalisimamie ipasavyo. Haki ni stahili ya mtu kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu zilizoelezwa vizuri katika kiapo chenu. Pia, vitabu vitakatifu vinasisitiza mkaamue kwa haki kati ya mtu na jirani na mgeni, mkasikilize wadogo na wakubwa sawasawa, msiangalie uso wa mtu yeyote kwa kuwa hukumu ni ya Mungu. Msiende kupindisha sheria, sheria ni nzuri kama itatumika kwa halali,” alisema Dk Mpango.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma alisema ongezeko la majaji hao 22 litapunguza mzigo wa mashauri wanayobeba kila mwaka.
Profesa Juma alisema kabla kila jaji alikuwa na mashauri wastani 340 baada ya uteuzi na uapisho huo yatashuka hadi 265.
“Nakupongeza kwa kuzingatia uwiano wa jinsia kwa sababu kabla ya uteuzi majaji wanawake Mahakama Kuu walikuwa ni 27 sawa na asilimia 35 kati ya 78 baada ya uteuzi asilimia imepanda hadi 37. Si haba imeongezeka,” alisema.
Majaji wa Mahakama kuu walioapishwa jana ni Kevin Mhina, Gabriel Malata, Happiness Ndesamburo, Ruth Massam, Adrian Kilimi, Godfrey Isaya, Obadia Bwegoge, Victoria Nongwa, Gladys Barth, Fatma Khalfan, Asina Omari na Hamidu Mwanga.
Majaji wengine wa Mahakama Kuu ya Tanzania walioapishwa jana ni Merlyn Komba, Monica Otaru, Kamana Kamana, Lusungu Hongoli, Suleiman Hassan, Mwajuma Juma, Dk Cleophace Kassenene, Aisha Bade na Musa Pomo.