RAIS Samia Suluhu Hassan amewatakia heri watahiniwa wa mitihani ya Kidato cha Sita iliyoanza jana.
Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter, Rais Samia ameeleza kuwa taifa linawaamini na linawategemea wanafunzi hao.
“Naamini mmejiandaa vyema kwa hatua hii muhimu kwenye safari yenu ya elimu, na nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape utulivu na siha njema mkahitimishe salama na kwa mafanikio,” alieleza Rais Samia.
Aliongeza: “Serikali itaendelea kuhakikisha inaandaa mazingira bora katika safari yenu kuelekea hatua zifuatazo ikiwemo vyuo vya ufundi, vyuo vya kati na vyuo vya elimu ya juu.”
Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) limesema watahiniwa 106,955 wamesajiliwa kufanya Mtihani wa Kidato cha Sita (ACSEE).
Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Said Mohamed aliwaeleza waandishi wa habari kuwa katika mtihani huo watahiniwa wa shule ni 96,914 na wa kujitegemea 10,041.
Dk Mohamed alisema Dar es Salaam kuwa watahiniwa wanaume ni 53,324 sawa na asilimia 55 na wanawake ni 43,590 sawa na asilimia 45.
Alisema Mtihani wa Kidato cha Sita utafanyika katika shule 883 za sekondari na vituo 257 vya watahiniwa wa kujitegemea.
Dk Mohamed alisema Mtihani wa Ualimu utafanyika katika vyuo 95 vya ualimu vikiwa na watahiniwa 8,906 waliosajiliwa kufanya mtihani wa ualimu kwa ngazi ya stashahada na cheti.
“Katika mtihani wa ualimu kati yao 2,344 ni ngazi ya stashahada na watahiniwa 6,562 ni ngazi ya cheti. Kwa ngazi ya stashahada wanaume ni 1,438 sawa na asilimia 61 na wanawake ni 906 sawa na asilimia 39,” alisema.
Dk Mohamed alisema Necta imeziagiza kamati za mitihani za mikoa, halmashauri, manispaa na majiji kuhakikisha taratibu za uendeshaji zinazingatiwa.
“Kamati zihakikishe mazingira ya mitihani yanakuwa salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha kutokea kwa udanganyifu, kuimarisha usalama wa vituo teule na kuvisimamia kwa kuzingatia mwongozo uliotolewa na baraza hilo,” alisema.
Pia aliwataka wasimamizi wa mitihani kufanya kazi kwa kusimamia mitihani kwa unakini na uadilifu wa hali ya juu na wamiliki wote wa shule kutambua shule ni vituo maalumu hivyo hawatakiwi kwa namna yoyote ile kuingilia majukumu ya wasimamizi wa mitihani katika kipindi chote cha ufanyikaji wa mitihani.