RAIS Samia Suluhu Hassan amewaeleza wanafunzi wa Darasa la Saba kuwa serikali itahakikisha inakamilisha maandalizi ya miundombinu ya kuwapokea watakaoendelea na Kidato cha Kwanza mwakani. Rais Samia ameyasema hayo katika ujumbe aliotuma kuwatakia heri wanafunzi hao walioanza mitihani jana kuhitimu elimu ya msingi Tanzania Bara.
“Nawatakia kila la kheri wanangu wote mnaoanza mtihani wa darasa la saba leo (jana). Mwenyezi Mungu awape utulivu na siha njema ili mfanye vizuri mitihani yenu,” aliandika Rais Samia katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter.
Viongozi kadhaa akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Angella Kairuki na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa wamewatakia heri wanafunzi hao. Naibu Katibu Mkuu Tamisemi anayeshughulikia Elimu, Dk Charles Msonde amesema serikali imejipanga kusimamia mitihani hiyo kupitia viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa.
“Nimepita shule kadhaa katika Mkoa wa Dar es Salaam, hali ni nzuri wanafunzi wameanza kufanya mitihani yao vizuri kwa utulivu na watendaji wamejipanga kusimamia vizuri kama tulivyoelekeza, niendelee kusisitiza mitihani hii ifanyike kwa kuzingatia kanuni na taratibu,” alisema Dk Msonde.
Aliwataka wanafunzi wanaomaliza mitihani leo wasiwe na wasiwasi kwa kuwa mitihani hiyo inatungwa ndani ya mada walizofundishwa katika masomo hivyo waifanye kwa umakini na umahiri. Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) lilitangaza juzi kuwa wanafunzi 1,384,340 walitarajiwa kufanya mitihani hiyo katika shule 17,943 kwa siku mbili, jana na leo.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Necta, Athumani Amasi alisema watahiniwa watafanya mitihani katika masomo sita ya Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia, Hisabati, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi na Uraia na Maadili.
Amasi alisema idadi ya watahiniwa wa mwaka huu imeongezeka kwa asilimia 22.28 ikilinganishwa na mwaka jana ambao watahiniwa hao walikuwa 1,132,084.
Alisema kati ya watahiniwa 1,384,340, wavulana ni 661,276 sawa na asilimia 47.77 na wasichana ni 723,064 sawa na asilimia 52.23.
Amasi alisema watahiniwa 1,325,433 wanafanya mitihani hiyo kwa Lugha ya Kiswahili na watahiniwa 58,907 kwa Kiingereza.
Alisema watahiniwa wenye mahitaji maalumu wapo 4,221 na kati yao 101 ni wasioona, 1,198 ni wenye uoni hafifu, 962 wenye uziwi, 487 wenye ulemavu wa akili na 1,473 ni wenye ulemavu wa viungo mwilini.