Samia awataka viongozi kujitathimini wenyewe
SINGIDA: RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Wilaya ya Mkalama kujitathimini katika utendaji wao wa kazi ili kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo tangu kuanzishwa kwake miaka 11 iliyopita.
Rais Samia amesema hayo Oktoba 16, 2023 wakati akizindua daraja la Msingi Mkalama lenye urefu wa Mita 100, lililopo wilayani Mkalama Mkoa wa Singida.
Ameongeza fedha nyingi zimetumika katika ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kuvutio cha utalii hutumika pia katika usafiri na usafirishaji kwa kuunganisha Mikoa ya kanda ya kati na kanda ya ziwa, sambamba na kuinganisha nchi na maeneo ya mipakani ikiwemo mpaka wa Sirari, Kenya.
Aidha, Rais Samia amesema mbali na changamoto mbalimbali ambazo Serikali kuu inazishughulikia ikiwemo changamoto katika sekta ya elimu, lakini halmashauri pia inapaswa kushughulikia changamoto nyingine ikiwemo ujenzi wa vyoo.
“Upungufu wa walimu wa shule za msingi ni asilimia 40 na kitu.. na shule ya sekondari upungufu ni asilimia 26,” amesema Kiongozi huyo.
Aidha, akizungumzia kuhusu changamoto ya uhaba wa nyumba za walimu, Rais Samia amesema Bajeti ya mwakani ya Serikali itaenda kujikita zaidi katika kutatua changamoto hiyo.