Samia awataka Watanzania kuwekeza Msumbiji

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka Watanzania wanaoishi na kufanya biashara nchini Msumbiji kutumia fursa ya ushirikiano wa nchi hizo mbili kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.

Rais Samia aliyasema hayo alipozungumza katika ofisi za Manispaa ya Jiji la Maputo nchini Msumbiji Alhamis akiwa katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku tatu nchini humo.

Akiwa hapo, Rais Samia alipata heshima ya kukabidhiwa funguo ya Jiji la Maputo kama ishara ya heshima na ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji.

Alisema Serikali ya Tanzania inajua wazi kuna Watanzania wengi wanaoishi na kufanya biashara nchini Msumbiji, hivyo yeye na Rais Filipe Nyusi wamekubaliana kuwaeleza raia wao kushirikiana kwa faida ya nchi hizo mbili.

“Sisi Watanzania tunajua kwamba kuna Watanzania wengi wanaoishi na kufanya biashara Maputo, nikiwa na kaka yangu Nyusi tulikubaliana kuwaeleza watu wetu kushirikiana kufanya biashara na kuwekeza kwa manufaa ya nchi zetu,” alisema Rais Samia.

Akizungumzia kukabidhiwa funguo ya Jiji la Maputo na Meya wa jiji hilo, Eneas Comiche, Rais Samia alisema hiyo ni heshima kubwa kwake na anajisikia fahari kuwa kiongozi wa pili kutoka Tanzania kupokea funguo hiyo akitanguliwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

“Kwangu mimi hii ni heshima kubwa kama ambavyo Meya amesema kwamba mimi ni wa pili kutoka Tanzania kupokea funguo hii tangu Mwalimu Nyerere. Funguo hii ni muhimu na alama ya uaminifu, inamaanisha kwamba sina haja ya kuomba ruhusa ya kuja Maputo na mkiniona nikitembea Maputo mjue nimekuja kutembea nyumbani,” alisema Rais Samia.

Alimkaribisha Meya Comiche kutembelea Dar es Salaam na Dodoma ili akutane na wenzake washirikiane katika kutafuta suluhu ya changamoto walizozitaja.

Naye Meya Comiche alisema ufunguo waliomkabidhi Rais Samia ni ishara ya kufungua milango ya ushirikiano baina ya Msumbiji na Tanzania, kuuimarisha na pia kuhuisha kumbukumbu za wakati Mwalimu Nyerere alipotembelea nchi hiyo na mchango wake katika kupigania uhuru wa nchi hiyo.

Aliongeza kuwa raia wa Msumbiji hawawezi kusahau mchango wa Tanzania kwa nchi yao na aliwataka Watanzania wajisikie wako nyumbani wanapokuwa katika nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika.

Pia alisema ana hakika nchi hizo mbili zitashirikiana vema katika kutatua changamoto zinazotokana na kukua kwa miji, ongezeko la watu na mabadiliko ya tabianchi katika kutekeleza maendeleo endelevu kwa nchi hizo.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x