Samia azindua mradi wa vihenge, maghala

RAIS Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa vihenge na maghala ya kuhifadhia nafaka mkoani Manyara yenye uwezo wa kuhifadhi tani 40,000.

Uzinduzi huo umefanywa jana eneo la Makatanini na kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, vihenge na maghala hayo vimegharimu shilingi bilioni 19.

Akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa maghala hayo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema ujenzi wa maghala na vihenge vya kuhifadhi nafaka ni mpango mkakati wa serikali katika kuboresha hifadhi ya chakula.

Bashe alisema maeneo matatu yamejengwa vihenge na maghala ya kuhifadhia chakula ambayo ni Manyara, Rukwa na Katavi ambapo kwa ujumla maeneo hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 90,000.

Alisema hivi sasa nchi ina maghala ya kuhifadhi nafaka tani 250,000 na kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vihenge na maghala yote uwezo wa hifadhi utafikia tani 341,000.

Bashe alisema malengo ni kuwa ifikapo Desemba mwakani nchi iweze kuhifadhi nafaka tani 500,000 na kuwa vihenge na maghala hayo yamejengwa kwa teknolojia ya kisasa ya kuondoa unyevu kwenye nafaka ili kuzuia sumu kuvu.

“Lengo letu ni kwamba Aprili mwakani Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) waanze kununua mahindi kwa wakulima, mitambo ni ya kisasa hata kama nafaka zina unyevu, hukaushwa na kuzuia sumu kuvu,” alisema.

Aidha, katika hatua nyingine Rais Samia alizindua barabara ya lami ya Babati Mjini yenye urefu wa kilometa nane iliyogharimu zaidi ya shilingi bilioni 13.

Mradi huo uliowekwa jiwe la msingi mwaka 2018, umekuwa na manufaa kwa wananchi wa Babati kwa sababu umeondoa adha ya vumbi kwa wakazi na kuongeza muda wa wananchi kufanya biashara kwani pamoja na ujenzi wa barabara hiyo pia umeweka jumla ya taa 182 za barabarani.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x