Samia azitaka mahakama kutumia teknolojia ya kisasa

ARUSHA: RAIS Samia Suluhu Hassan amezitaka mahakama kutoka nchi wanachama 16 za Kusini na Mashariki mwa Afrika kutumia teknolojia za kisasa katika kusikiliza kesi na kutatua migogoro mbalimbali ya kibiashara inayojitokeza barani Afrika.
Kiongozi huyo amesema mahakama ni lazima zijipange kusuluhisha migogogro inayoibuka sasa, ambayo mingi inachagizwa na ukuaji wa kiwanda cha ubunifu na teknolojia.
Amiri Jeshi Mkuu ameyasema hayo wakati akihutubia mkutano wa ufunguzi wa Jukwaa la majaji wakuu wa nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (SEACJF), jijini Arusha leo Oktoba 23, 2023.
Mkutano huo wa siku tano umehudhuriwa na zaidi ya Majaji wakuu 300 kutoka nchi wanachama na watapata fursa ya kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo mkoani Arusha na maeneo ya jirani ikiwemo hifadhi ya taifa ya Serengeti ili kujionea maliasili zilizopo nchini Tanzania.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amewataka majaji hao kuzijengea uwezo Mahakama katika nchi hizo ili ziwe na uwezo wa kutatua migogoro kwenye eneo huru la biashara barani Afrika.