Samia, dunia wamlilia Malkia Elizabeth II

RAIS Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa familia ya kifalme kwa kifo cha Malkia Elizabeth II (96) wa Uingereza, aliyefariki juzi nyumbani kwake Balmoral, Scotland.

Katika salamu zake alizotoa juzi usiku, Rais Samia alisema amesikitishwa na taarifa za kifo hicho.

“Kwa niaba ya Watanzania wote, natuma salamu za pole kwa familia ya kifalme@RoyalFamily na raia wote wa Uingereza. Malkia atakumbukwa duniani kote kama nguzo ya amani, umoja na utulivu.” Rais Samia jana alikwenda kusaini kitabu cha maombolezo katika makazi ya Balozi wa Uingereza nchini, Oysterbay, Dar es Salaam.

Malkia Elizabeth alifariki juzi wakati akiendelea na matibabu akiwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa siku kadhaa baada ya afya yake kuzorota.

Habari kutoka kwenye kasri ya kifalme Buckingham, ilisema hali ya Malkia ilibadilika ghafla hatua iliyofanya familia yake kukutana kwa dharura nyumbani kwake Balmoral, Scotland. Kutokana na kifo hicho, kiti cha ufalme kitachukuliwa na mtoto wa Malkia Elizabeth, Prince Charles (73) ambaye jana amerejea London. Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truss alitoa taarifa ya kifo muda mfupi baada ya familia ya malkia kutangaza kifo.

“Taifa lote limeshtushwa na tukio hilo…Malkia alikuwa msingi imara, Uingereza ya sasa imesimama.” Ikulu ya Marekani ilitoa salamu za pole na kusema kipindi chote cha utawala, Malkia Elizabeth alifanya mengi.

Ilisema upendo na busara zake watazikumbuka na kwamba alikutana na marais 14 wa Marekani.

Rais Joe Biden alisema kutokana na kifo hicho, bendera ya Marekani ndani na nje ya nchi itapepea nusu mlingoti kama kumbukumbu yake hadi siku atakapozikwa malkia huyo.

Mfalme Felipe wa Uhispania, kupitia ukurasa wake wa telegramu ameipa pole familia ya kifalme akisema wataendelea kumkumbuka. Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani alisema Malkia Elizabeth II ni alama ya dunia, mfano wa kuigwa na mtoa hamasa kwa mamilioni ya watu wakiwamo Wajerumani hususani kwa kufanikisha maridhiano ya Ujerumani na Uingereza baada ya vita kuu ya dunia.

Waziri Mkuu wa Canada, Justin Trudeau alimtaja kuwa alikuwa katika maisha ya watu kwa kusaidia na Canada itaendelea kubaki na historia yake. Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi katika ukurasa wake wa Twitter amemuelezea Malkia kama kiongozi aliyejali utu na kuheshimu maisha ya watu.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin alimpa pole mfalme wa Uingereza, Charles na Waingereza akiwataka wawe wastahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi. Mkuu wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen katika ujumbe wake alisema: “Malkia Elizabeth II alishuhudia vita pamoja na maridhiano, huku akiwa nguzo kuleta mabadiliko katika jamii na ulimwengu kwa ujumla.” Viongozi wengine duniani waliotoa salamu za pole ni pamoja na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Anthonio Guterres, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa na Rais wa Ghana, Nana Akufo-Ado.

Utaratibu unaosubiriwa ni ratiba ya mazishi.

Tangu juzi wananchi wa Uingereza walikusanyika nje ya kasri la Malkia Elizabeth II wakiomboleza kifo chake. Malkia Elizabeth wa pili amevunja rekodi ya kutawala kwa muda mrefu zaidi katika taifa hilo akilipitisha katika nyakati nzuri na za mapito kwa miaka 70.

Habari Zifananazo

Back to top button