Samia: Kigoma itakuwa kituo cha utalii wa tiba

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Kigoma utakuwa kituo cha utalii wa tiba na ametoa shilingi bilioni tano za kuanza ujenzi wa hospitali ya kanda.
Alisema hayo jana baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Maweni ambayo baadhi ya majengo ya huduma yamekamilika.
Rais Samia alisema serikali imeamua kuufanya Mkoa wa Kigoma kitovu cha biashara kwa ukanda huo hivyo inaendelea kuujenga sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara, maji, afya, elimu na nyingine ili kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana.
Alisema kuwa Kigoma inakuwa kitovu cha biashara hivyo lazima serikali iandae na kuweka kituo cha afya ili wageni na wenyeji wanapoendelea na uwekezaji na biashara wakiugua watibiwe hapo.
“Sisi maono yetu tuwe na utalii wa afya, watu watoke nchi jirani waje kupata huduma za tiba hapa. Tanzania iwe kituo cha ubingwa wa mambo ya afya kwa nchi tunazopakana nazo, ndio maana nimetoa tena hizo Sh bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya kanda hapa Kigoma,” alisema Rais Samia.
Alisema Kigoma ni mkoa wa pembezoni mwa nchi na sasa wameufanya mkoa wa kimkakati wa biashara ndio maana serikali imehakikisha unapata umeme wa gridi wa uhakika ili ufungue fursa za uwekezaji.
Awali akizungumza mara baada ya kutembelea ujenzi wa hospitali ya Maweni, Rais Samia alisema baadhi ya majengo yamekamilika na vifaa tiba vipo na huduma zitaanza kutolewa Novemba Mosi.
“Nimetembelea majengo ya hospitali hii ya rufaa ya Maweni, tumeamua kukuza hospitali hiyo kwa kuwa Kigoma ina watu wengi. Awali mkoa ulikuwa unatumia fedha nyingi kufuata baadhi ya huduma za tiba Hospitali ya Bugando (Mwanza) na kwingine, lakini sasa kwa ujenzi huu huduma hizi zinatolewa hapa hapa,” alisema Rais Samia.
Alisema ametembelea baadhi ya majengo katika hospitali hiyo na kuona vifaa tiba kama CT- Scan na huduma nyingine na zitatafutwa fedha kukamilisha majengo.
“Nimezungumza na waziri tutafute bilioni mbili tuzilete hapa tumalizie majengo ambayo nimeona yananing’inia pale pembeni ili yamalizike, sura iwe nzuri,” alisema Rais Samia.
Aidha, aliwashukuru watumishi wa hospitali ya Maweni kwa kazi wanayofanya ya kuhudumia wagonjwa na akasema Mungu atawalipa zaidi kwani serikali haiwezi kuwalipa kwa huduma wanazotoa.
“Mnachokipata serikalini ni kidogo hakuna serikali inayoweza kuwapa, ila kikubwa Mungu anajua jinsi ya kuwapa kipato zaidi. Mama yenu silali, nachapa kazi na nyie msilale chapeni kazi tuijenge nchi,” alisema Rais Samia.