RAIS Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuhudhuria katika sherehe za kuadhimisha miaka 10 ya Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).
Rais mstaafu, Dk Jakaya Kikwete pia anatarajiwa kuwa mzungumzaji mkuu katika kongamano la kwanza la wanachuo wa chuo hicho.
Hayo yalibainishwa jijini Dar es Salaam Jumatano na Kamanda wa NDC Meja Jenerali Ibrahim Mhona, alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya hafla hiyo kubwa.
Meja Jenerali Mhona alisema kuwa Rais atahudhuria sherehe za chuo hicho ambacho kimekuwa na nafasi ya kipekee katika kutoa kozi za usalama na mikakati kwa viongozi wa Tanzania na viongozi kutoka nchi nyingine za Afrika.
“Rais Samia ndiye atakuwa mgeni wetu rasmi, ambapo atapata nafasi ya kusikiliza taarifa fupi ya utendaji kazi wa NDC, ambapo chuo kimetoa mafunzo ya amani na usalama, si kwa viongozi wa Tanzania pekee bali hata kwa viongozi kutoka nchi nyingine za Afrika. ” alisema Kamanda.
“Rais pia atapokea ripoti ya jinsi NDC ilivyokuwa kinara wa amani Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kupitia kudahili na kutoa mafunzo kwa wajumbe wa vyombo vya usalama na watumishi wa umma kutoka nchi hizo,” alisema.
Alieleza baadhi ya hatua zilizofikiwa na NDC, ambapo takriban maofisa 435 kutoka vyombo vya usalama na watumishi wa umma kwa miaka kumi iliyopita wamehitimu mafunzo ya stashahada na shahada ya uzamili katika chuo kikuu katika masomo ya ulinzi na usalama.
Chuo hicho pia kinaendesha kozi za kuwanoa maofisa wakuu wa serikali na vyombo vya usalama wa taifa mara mbili kila mwaka kwa lengo la kudumisha amani na usalama ikiwa ni hatua muhimu ya maendeleo ya kiuchumi.
Meja Jenerali Mhona alisema hadi sasa maafisa wasiopungua 574 wamehudhuria kozi za msingi katika chuo hicho.
Katika kuadhimisha miaka kumi tangu kuanzishwa kwake, NDC Jumatano ilifanya zoezi la upandaji miti pamoja na kusafisha mazingira yanayozunguka fukwe za Dar es Salaam.
NDC iliyoanzishwa mwaka wa 2011, ndiyo taasisi ya juu zaidi ya kujifunza kimkakati na taasisi kuu ya mafunzo ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kitaifa.