Samia kuhutubia miaka 59 Uhuru wa Zambia

DAR ES SALAAM: Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 59 ya Uhuru wa Jamhuri ya Zambia zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 24, 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya bara la Afrika.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba amesema Rais Samia amealikwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe hizo na Rais wa Zambia Hakainde Hichilema.
Rais Samia pia amealikwa kufanya Ziara ya Kitaifa nchini Zambia kuanzia Oktoba 23 – 25 ,2023 ambapo pamoja na mambo mengine, atakuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Kongamano la Biashara kati ya wafanyabishara wa Tanzania na Zambia.
“Ziara hii ni ya kwanza ya Kitaifa ya Rais kufanya nchini Zambia tangu alipohudhuria uapisho wa Rais Haichilema mwaka 2022, itakumbukwa kuwa Tanzania na Zambia zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu ambao umejengwa na misingi ya kindugu,” amesema Makamba.
Waziri Makamba amesema Rais Samia pia amepewa heshima ya kuhutubia Bunge la Jamhuri ya Zambia tarehe 25 Oktoba, 2023 na anakuwa kiongozi mashuhuri wa wanne kuhutubia Bunge hilo.

Habari Zifananazo

Back to top button