RAIS Samia Suluhu Hassan kesho anatarajiwa kuongoza Mkutano wa 14 wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) utakaofanyika Ikulu ya Magogoni, Dar es Salaam.
Katibu Mtendaji wa TNBC, Dk Godwill Wanga aliwaambia waandishi wa habari kuwa maandalizi ya mkutano huo yameshakamilika na wajumbe wa mkutano huo wamewasili Dar es Salaam.
“Kaulimbiu ya mkutano huu ni ‘Mazingira Bora ya Biashara kwa Uchumi Himilivu na Shirikishi’,” alisema Dk Wanga.
Alisema moja ya mambo yatakayojadiliwa ni kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (MKUMBI) nchini, ambao wajumbe watapata fursa ya kujadili mafanikio, changamoto na mapendekezo ya maboresho ya utekelezaji wake.
“Kadhalika mkutano utaeleza jinsi serikali inavyoshirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha nchi kiuchumi,” alisema Dk Wanga.
Alisema wajumbe wa TNBC pia watapata nafasi ya kupitia ripoti za utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika Mkutano wa 13 wa TNBC ambao ulifanyika Dodoma, Juni 7 mwaka jana.
“TNBC chini ya uenyekiti wake Dk Samia, imepata mafanikio makubwa ikiwemo kuimarika kwa mahusiano na kuaminiana baina ya sekta za umma na binafsi sambamba na kufunguka na kuimarika kwa nchi kibiashara na uwekezaji,” alisema Dk Wanga.
Dk Wanga alisema mazingira ya biashara na uwekezaji yameendelea kuboreshwa nchini. Alisema vikwazo vingi vya kufanya biashara na uwekezaji vimeondolewa na kwa sababu hiyo Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia inaaminiwa na wafanyabiashara na wawekezaji ndani na nje ya nchi.
“Mabaraza ya Biashara ya Wizara, Mikoa na Wilaya yamekuwa chachu kubwa ya kuibua fursa za kibiashara na uwekezaji katika uchumi wetu. Na kupitia mabaraza hayo kero, tozo na makato mbalimbali yaliyokwaza biashara na uwekezaji zimetatuliwa,” alisema.
TNBC kimekuwa ni chombo muhimu cha majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi katika kufikia maazimio ya pamoja kuhusu masuala ya kuchochea biashara, uwekezaji kwa ajili ya kukuza uchumi na maendeleo ya kijamii kwa ajili ya mustakabali wa ustawi, maslahi mapana na maendeleo jumuishi ya taifa.