Samia: Mkataba bandari unaenda kuongeza mapato
DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema mikataba iliyoingiwa kati Serikali na kampuni ya DP World ya nchini Dubai, inaenda kuongeza mapato ya serikali, hivyo kukuza uchumi wa taifa.
Amesema bandari ya Dar es Salaam ni lango la biashara kwa nchi zinazozunguka, hivyo ni wajibu kuwekeza, kuboresha na kuhudumia nchi zinazoizungukaTanzania kama nyenzo ya kiuchumi pia kwa kuzingatia mkataba wa Umoja wa Mataifa (UN), unazozitaka nchi za mlango bahari kuhudumia nchi nyingine.
Amesema hayo leo Oktoba 22, 2023, Ikulu ya Chamwino, Dodoma katika hafla ya utiaji saini wa mikataba mitatu ya uendelezaji na uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, kati ya Serikali ya Tanzania chini ya Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) na Kampuni ya DP World ya nchini Dubai.
Amesema mchakato wa majadiliano ya uingiaji mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na DP World katika uendelezaji na uendeshaji wa bandari ya Dar es Salaam umekuwa shirikishi tangu mwanzo wa majadiliano mpaka sasa katika uingiaji wa mkataba wa utekelezaji.
“Kwa uhakika hakuna sauti au kundi ambalo halikusikilizwa au lilipuuzwa. Serikali tuliunda jopo la wataalamu, pia wanasiasa na wanasheria waangalie hoja zote na watuambie ipi iingie kwenye mkataba na ipi haina mashiko.
“Mikataba hii imezingatia maoni yote yaliyotolewa, maslahi mapana ya nchi yetu yamezingatiwa,” amesema Rais Samia.