Samia: Muungano unahitajika leo, ulindwe

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Muungano wa Tanzania umeliimarisha taifa, na kwamba unahitajika leo kama ambavyo ulihitajika mwaka 1964 ulipoasisiwa.

Amesema Muungano huo wa Tanganyika na Zanzibar ni maalumu na wa kipekee uliojengwa kwenye misingi ya utu, udugu na umajumui wa Afrika. Akihutubia taifa jana katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano inayosherehekewa leo, Rais Samia alisema hakuna wa kuuvunja Muungano kwani umeshinda majaribu mengi ya kuuvunja lakini umedumu mpaka sasa. Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulifanyika Aprili 26, 1964 kwa Rais wa Tanganyika, Julius Nyerere na Rais wa Zanzibar, Abeid Amani Karume.

Mwalimu Nyerere akishirikiana na vijana wanne, wawili wa kike na wawili wa kiume walichanganya udongo wa pande hizo mbili na kuzaliwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Ninapohitimisha hotuba yangu, niseme tu kwamba, Muungano wetu umetuimarisha zaidi kama Taifa, na kwamba Muungano wa Taifa letu unahitajika leo, kama ambavyo tuliuhitaji mwaka 1964.

“Hivyo basi, hatuna budi kuulinda Muungano huu kwa manufaa ya Watanzania wa kizazi cha sasa na Watanzania wa vizazi vijavyo,” alisema Rais Samia.

Aliongeza: “Jinsi udongo ulivyo, ni vigumu sana kuuchambua na kuweza kuutenganisha uliotoka Zanzibar na ule uliochotwa Tanzania Bara. Baada ya kuuchanganya, hakuna teknolojia inayoweza kuurudisha udongo ule kwenye hali yake ya awali katika vibuyu viwili tofauti. Kwa maana nyingine, kitendo cha kuchanganywa kwa udongo kiliashiria dhamira ya kujenga muungano wa kudumu”.

Akinukuu maneno ya Mwalimu Nyerere, Rais Samia alisema: “Nyerere aliwahi kusema maneno yafuatayo, ‘Tanzania ni lulu ya pekee kabisa katika historia ya Afrika huru. Nchi nyingine zote ni za kurithi kutoka katika Ukoloni, lakini Tanzania ni ya kuundwa na sisi wenyewe, kwa hiari yetu wenyewe, baada ya kukomboa sehemu (zote mbili za Muungano) kutoka katika Ukoloni’.”

Rais Samia alisema kwa upande wake, Sheikh Abeid Amani Karume akiuzungumzia Muungano huu, aliwahi kusema, nanukuu: ‘Muungano wa Tanganyika na Zanzibar una thamani kubwa kwetu sisi Waafrika’.’’

Alisema anamshukuru Mungu kwa kuinasibisha historia ya maisha yake na muungano kwani pamoja na kuyaishi masuala ya Muungano kama raia wengine, amebahatika pia kufanya kazi katika kuuimarisha Muungano kama Mjumbe wa Kamati ya Pamoja ya kutatua Changamoto za Muungano, Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais wa Tanzania anayeshughulikia masuala ya Muungano, Makamu wa Rais na sasa Rais.

Alisema inawezekana baadhi ya Watanzania wakajiuliza iliwezekanaje muungano ukawepo, na umewezaje kudumu miaka yote hii.

“Majibu ya maswali hayo ni muhimu kwa kutambua kwamba zaidi ya robo tatu ya Watanzania wa leo, wamezaliwa baada ya Muungano. Maelezo kuhusu maswali hayo yapo mengi, lakini kwa muktadha wa leo nitazungumzia mambo makubwa matatu yaliyoufanya Muungano wetu udumu na kuimarika,” alisema Rais Samia.

Aliyataja mambo hayo matatu yaliyoimarisha Muungano kuwa ni imani na dhamira ya dhati waliyokuwa nayo waasisi Nyerere na Shehe Karume, udugu wa kihistoria, na umadhubuti wa viongozi waasisi waliotanguliza mbele maslahi ya watu na taifa.

Alisema sababu nyingine ya muungano kudumu ni uwepo wa Tume ya Pamoja chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais inayosikiliza na kutatua changamoto za Muungano kila zinapojitokeza. “Kati ya mwaka 2021 hadi sasa, hoja 15 kati ya 18 zimeshapatiwa ufumbuzi.

Tume hiyo inafanya kazi kubwa ya kulinda dhamira ya dhati ya kuudumisha Muungano wetu… lakini muungano pia umetuwezesha kulinda Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, lakini pia kwa umoja wetu, na kupitia jeshi letu, tumeweza kulinda mipaka ya taifa letu,” alifafanua Rais Samia.

“Nina furaha leo kuwahakikishia kwamba mipaka yetu, uhuru wetu na mapinduzi yetu, vyote viko salama ndani ya Muungano wetu. “Nafarijika kwamba Jeshi letu la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ifikapo Septemba mwaka huu nalo linatimiza miaka 60 tangu kuundwa kwake,” alieleza.

Alisema jitihada zilizofanywa ndani ya miaka 60 zimesaidia kukuza Pato la Taifa kufikia Sh trilioni 170.3 kwa takwimu za mwaka 2022, na pato la mtu mmoja mmoja kufikia wastani wa Sh milioni 2.8 kwa mwaka 2022.

“Nafarijika kwamba, kwa sasa nchi yetu imefikia uchumi wa kati, katika ngazi ya chini na jitihada zetu zote sasa ni kufikia uchumi wa kati, ngazi ya juu. Vilevile, wastani wa umri wa kuishi wa Mtanzania umeongezeka kutoka miaka 45 mwaka 1964 hadi miaka 67 mwaka 2024,” alieleza.

Alisema suala la usawa wa kijinsia limepewa umuhimu katika muungano tangu siku ya kwanza ya muungano na kwamba siku za nyuma hapakuwa na mwanamke yeyote kwenye uongozi wa mihimili ya dola, Serikali, Bunge na Mahakama.

“Leo hii, kati ya mihimili mitatu ya dola, wanawake wanaongoza mihimili miwili, Serikali na Bunge, jambo linalothibitisha kuendelea kuimarika kwa usawa wa kijinsia,” alisema.

Aliwasihi vijana wote wa Tanzania wawe walinzi wa Muungano, wakikumbuka kuwa wa Muungano huu ni urithi na tunu ya taifa na ni tunu ya Afrika kwa ujumla.

Kwa wanasiasa, Rais Samia alitoa wito kwao kukumbuka kwamba Muungano ni wa watu, hivyo siasa zijikite kwenye kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano, na kudhamiria kufanya siasa zenye kuleta maendeleo, kuwaunganisha watu, kuthaminiana, na kudumisha misingi ya utawala wa sheria.

Leo kwenye Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam kutafanyika sherehe za kilele cha miaka 60 ya Muungano ambako Rais Samia atakuwa mgeni rasmi.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi alisema viongozi wa nchi kadhaa wamethibitisha kuhudhuria akiwemo Rais wa visiwa vya Comoro, Azali Assoumani, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye.

Wengine ni Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Kenya, William Ruto, Rais wa Namibia, Nangolo Mbumba na Makamu wa Rais wa Malawi, Saulos Chilima.

Viongozi wengini ni Makamu wa Rais wa Uganda, Jessica Alupo, Waziri Mkuu wa Msumbiji, Adriano Afonso Maleiane, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje na Uhusiano wa Kikanda wa Rwanda, James Kabarebe, Katibu wa Masuala ya Nje wa Chama cha ZANU-PF cha Zimbabwe, Simbarashe Mumbengegwi na Rais wa Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB), Dk Akinwumi Adesina.

Habari Zifananazo

Back to top button