Samia, Ruto wakubaliana mambo 10
RAIS Samia Suluhu Hassan na Rais wa Kenya, Dk William Ruto wamewaagiza mawaziri wao kuhakikisha ifikapo Desemba mwaka huu, wawe wamekuja na majibu ya kero 14 za biashara zilizobakia baina ya nchi hizo.
Aidha, wamewaagiza kuharakisha mchakato mzima wa utekelezaji wa mradi wa kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa na Nairobi.
Katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili ya Rais Dk Ruto nchini, marais hao walikubaliana kuongeza ushirikiano katika maeneo takribani 10 yakiwamo ya biashara, kilimo, madini, utalii, mawasiliano, udhibiti vitendo vya kihalifu, mradi wa gesi asilia, kushirikiana kikanda na kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa mipaka.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukamilisha mazungumzo yao Ikulu ya Magogoni Dar es Salaam jana, Rais Samia alisema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano wa kibiashara.
Alisema kazi hiyo ilianza tangu kipindi cha Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye walikubaliana kuwataka wataalamu wa nchi hizo kufanyia kazi vikwazo vilivyokuwapo vya kibiashara vya Kenya na Tanzania.
Alisema wataalamu hao walitambua vikwazo 68 na kufanyia kazi 54 visivyo vya kikodi na sasa kuna vikwazo 14 vimebaki.
“Ndio maana tumewataka mawaziri wetu wa Biashara na Uwekezaji wakutane kwa haraka na kufanyia kazi vikwazo hivi ili tuwe na uhuru mpana wa kufanya biashara,” alisema Rais Samia mbele ya Dk Ruto.
Hata hivyo, alisema kazi iliyoanza ya kufanyia kazi vikwazo hivyo vya biashara, imekuza biashara baina ya nchi hizo kwa kiasi kikubwa na Tanzania imefaidika mara mbili zaidi ya ilivyokuwa ikifaidika.
“Rais Ruto wakati anazungumzia hili alisema ikifaidika Tanzania na Kenya pia imefaidika. Kwa sababu Kenya na Tanzania tusigawane umasikini na udhalili lakini tugawane utajiri tutakaoupata kupitia biashara,” alisema.
Alitaja maeneo mengine waliyokubaliana kushirikiana kuwa ni kukuza uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo kwa kuwa ukiacha mipaka ya kiutawala, lakini kwenye mambo mengine nchi hizo ziko pamoja.
Eneo lingine walilokubaliana ni Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano uliokuwa ufanyike Agosti, mwaka huu na kuwaagiza mawaziri wa Mambo ya Nje wakutane na kujadili masuala yanayohusu mkutano huo.
Kuhusu kuimarisha mpaka wa kimataifa baina ya Kenya na Tanzania, alisema wamekubaliana kutekeleza jambo hilo ili kuwarithisha watoto wa nchi hizo kwa kujua mipaka ya nchi zao ya kiutawala imepita wapi.
Alisema tayari awamu ya kwanza imeshafanyika na kuwataka wataalamu wa nchi hizo kukutana na kuangalia uwezekano wa kuanza utekelezaji wa awamu ya pili.
Aidha, alisema pia kuhusu mradi wa kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es Salaam hadi Mombasa, ambao tayari ulishasainiwa na Uhuru wamekubaliana kuwa ndio mradi ambao Dk Ruto ataanza kuufanyia kazi.
Alieleza kuhusu kushirikiana kudhibiti vitendo vya kiuhalifu kwa kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kushirikiana kwa karibu na kuzungumza kuangalia makosa yanayovuka mipaka ya dawa za kulevya, maharamia, ujangili na usafirishaji wa binadamu.
Pia, marais hao wamekubaliana kushirikiana katika masuala ya kikanda na kimataifa kwa kuendeleza ushirikiano madhubuti kwenye Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa na hasa ndani ya Afrika Mashariki.
Kwa upande wake, Dk Ruto alizungumzia kuondoa vikwazo vya biashara baina ya Tanzania na Kenya na kueleza kuwa wakati vikwazo hivyo vikifanyiwa kazi, watu wengi walidhani vitainufaisha zaidi Kenya, lakini hii leo, Tanzania imenufaika zaidi kuliko Kenya.
Alisema tangu vikwazo hivyo vishughulikiwe biashara baina ya nchi hizo imekua ambako Kenya imeuza bidhaa za Sh bilioni 45 kutoka Sh bilioni 31 wakati Tanzania imeuza Kenya bidhaa za Sh bilioni 50 kutoka bidhaa za Sh bilioni 21 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.
“Nimekuja kukuhakikishia na kuwahakikishia Watanzania kwamba, msingi wa ushirikiano uliojengwa kati yako (Rais Samia) na mtangulizi wangu, Rais Uhuru Kenyatta nitauendeleza,” alisema Dk Ruto aliyeshinda Uchaguzi Mkuu wa Kenya wa Agosti 9, mwaka huu.
Aliwaagiza wataalamu wa nchi hizo mbili kupitia vikwazo hivyo 14 vilivyobaki na kuhakikisha hadi ifikapo Desemba mwaka huu, viwe vimefanyiwa kazi ili watu wa pande zote mbili wafanye biashara kwa uhuru.
“Nawathibitishia kuwa mawaziri wetu kazi yao itakuwa ni kufanya kazi na mawaziri wa Tanzania ili kuondoa vikwazo hivi, wakati tunaenda kwenye Sikukuu ya Krismasi biashara iwe inafanyika kwa uhuru. Tunataka biashara ikue kwa manufaa ya Kenya na Tanzania,” alisisitiza Dk Ruto.
Alitaja maeneo mengine waliyokubaliana kushirikiana ni bomba la gesi asilia na kuahidi kuwa serikali yake itaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji katika mradi huo ili ukamilike kwa wakati na Kenya ianze kutumia gesi hiyo itakayokuza sekta ya viwanda nchini humo.
“Lakini pia tumekubaliana kushirikiana katika mambo ya utalii. Nchi zetu zote zina rasilimali za kutosha za utalii. Tuna wanyama wanaokwenda Tanzania na wanaokuja Kenya tena bila pasipoti. Tunataka ushirikiano wa nchi zetu uwe wa uhuru kama hawa wanyama,” alieleza.
Eneo lingine alilotaja la ushirikiano ni mawasiliano kupitia Mtandao Mmoja wa Afrika Mashariki ambao nchi nyingine za jumuiya hiyo kama vile Rwanda, Uganda na Sudan Kusini nazo zimeridhia.
“Tunaamini katika kuendeleza mambo ya mawasiliano. Tukiwa na mtandao mmoja wa mawasiliano biashara na undugu itaongezeka na nchi zetu zitanufaika na wananchi watawasiliana kwa gharama ya chini,” alisema Dk Ruto.
Pia alisema wamekubaliana na Kamisheni ya Pamoja ili kila kilichozungumzwa katika ziara hiyo kitiwe saini jambo litakalosaidia utekelezaji wake ufanyike kikamilifu.
“Nataka niwaambie Watanzania mko na marafiki, ndugu kutoka Kenya. Najua hapa Tanzania kuna ma-hustler wengi ila mimi ndio master (mkubwa) wao,” alisisitiza.
Rais Ruto amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku mbili nchini ikiwa ni ya kwanza Tanzania kufuatia mwaliko wa Rais Samia. Amerejea nyumbani jana mchana.