Samia Scholarship yaleta mwamko sayansi kwa wasichana

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema mpango wa Samia Scholarship kwa wanafunzi waliofanya vizuri masomo ya sayansi umeleta mwamko na ushindani mkubwa kwa watoto wakike kuvutiwa kusoma masomo hayo.

Profesa Mkenda alisema hayo juzi wakati wa mkutano wa 23 wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe Mkoani Morogoro .

Waziri Profesa Mkenda alisema kuwa , Samia Scholarship inaendelea vizuri zaidi na imehimiza watoto wa darasa la saba kwa kuambizana wasome kwa bidii ili kuwapunguzia wazazi wao mzigo .

“ Najua sasa hivi wanafunzi wengi wanasema na mimi ninataka kwenda kusoma sayansi kwa sababu kuna Samia Scholarship..hili ni jambo zuri linalifanyika chini ya Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan na tunaridhika nalo “ alisema Profesa Mkenda

Waziri Profesa Mkenda alisema , Serikali imeanzisha Samia Scholarship kwenye masomo ya sayansi , na kamba anayefanya vizuri zaidi ndiye anayepata ufadhili , haijalishi ni mtoto wa nani na kinachoangaliwa kufanya vizuri katika masomo hayo na atapata fursa ya kusomeshwa .

Profesa Mkenda alisema, Samia Scholarship itagharamia kwa asilimia mia moja masomo ya Elimu ya Juu kwa wanafunzi hao ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba.

Hivyo Serikali kupitia Wizara hiyo inatarajia kutumia Sh bilioni sita kutoa ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kwa mwaka 2023/24 kupitia Mpango wa Samia Scholarship kwa wahitimu wa kidato cha Sita wapatao 640.

Waziri Profesa Mkenda alisema ,hivi sasa serikali kupitia wizara inafikiria kuanzisha mpango mwingine wa Samia Scholarship International.

Alisema utaandaliwa mwongozo kwa ajili ya kuwawezesha wenye ufaulu wa juu katika shahada ya kwanza nay a pili ya sayansi ya udaktari ( Medicine) kwenda kusoma vyuo vikuu vya nje ya nchi.

Mbali na hayo Profesa Mkenda, alivitaka vyuo vikuu nchini kutenga fedha kwa ajili ya tafiti zitakazo saidia kutatua changamoto za jamii ya Tanzania.

Alisema ,kwa upande wa serikali imeanza kutenga fedha kwa ajili kuendeleza sayansi uhandisi pamoja na tiba ikiwa na kuandaliwa mazingira wezeshi ya kuongeza nguvu katika matumizi ya Tehama , ili kuendana na kasi ya utandawazi

Pamoja na hayo , Waziri Profesa Mkenda alisema kwa mwaka wa fedha 2022/23 Serikali imetenga kiasi cha sh milioni 500 kwa Chuo Kikuu Mzumbe ili kuboresha miundombinu ya Chuo hicho.

Kwa upande wake Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha alisema Chuo kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kukamilisha ujenzi wa hostel ambazo zitabeba zaidi ya wanafunzi 1,026.

Pia alisema kwa miaka mitano kuanzia 2018/2019 kumekuwa na ongezeko kwa udahili wa wanafunzi kutoka 11,694 hadi 13,718 kwa kampasi zote ambalo ni ongezeko la asilimia 17.3 na kwamba kwa mwaka huu wa masomo , Chuo kinatarajia kudahili wanafunzi 15,000.

Katika hatua nyingine alisema chuo kimenzisha harambee malaumu ya kukusanya fedha bilioni 5.8 kwa ajili ya kujenga jengo la hoteli ya wanafunzi wa kike lenye uwezo wa kulaza wanafunzi 800 kampasi ya Mbeya .

Habari Zifananazo

Back to top button