Samia: Soko Afrika linufaishe wanawake, vijana

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia.

RAIS Samia Suluhu Hassan amezitaka nchi za Afrika zitoe kipaumbele katika maeneo yanayogusa wanawake na vijana wakati wa utekelezaji Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ili kuwainua kibiashara na kiuchumi.

Ameagiza kuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa mkataba huo yafunguliwe masoko katika sekta muhimu ambazo wanawake na vijana wanajishughulisha nazo kikiwemo kilimo, viwanda vya nguo, usindikaji wa mazao ya kilimo, huduma na kuzingatia utalii na biashara nyingine.

Rais Samia alisema hayo Jumatatu Dar es Salaam wakati akishiriki Kongamano la Wanawake na Vijana la AfCFTA.

Advertisement

“Serikali ya Tanzania na mimi binafsi tumejipanga kuhakikisha wanawake na vijana wananufaika ipasavyo na mipango na mikataba tunayokwenda kuitekeleza. Katika serikali hii wako wanawake wengi katika serikali za juu na wote wameonesha kiwango kikubwa cha uongozi na ninawataka wakawajibike kwenye maeneo haya,” alisema.

Aliongeza: “Wote wanawake na viongozi wa Tanzania Bara na Zanzibar muende mkawajibike kila mmoja alipo kwenye maeneo hayo.”

Rais Samia alisema kama kaulimbiu ya kongamano hilo inayosema: Wanawake na Vijana ni Injini ya Biashara chini ya mkataba wa eneo huru la biashara Afrika, wanawake na vijana huwekeza zaidi kwa ajili ya familia zao katika maeneo ya elimu, afya na lishe hivyo kuwawezesha kiuchumi kunatengeneza fursa za uhakika za ajira kwa kila mtu na uimara wa Taifa kwa ujumla.

Alisema Ajenda ya mwaka 2063 ndoto yake ni kuwa na Afrika iliyofanikiwa, kustawi na yenye nguvu na amani, hivyo ni jukumu la wote kufanya mabadiliko ya kiuchumi Afrika ili kuleta maisha bora kwa Waafrika na ili hayo yatokee ni lazima kuwajengea uwezo wanawake na vijana kushiriki kikamilifu na kutumia fursa zitokanazo na soko la Afrika.

Rais Samia alisema ili kushirikisha wanawake na vijana katika biashara, nchi za Afrika kupitia majadiliano ya eneo huru la Afrika zilikubaliana kuanzisha Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara.

Alisema ana imani itifaki itakayoandaliwa itaainisha fursa za kisera zitakazosaidia wanawake na vijana kunufaika na soko huru la biashara Afrika.

“Ni matumaini yangu itifaki ya wanawake itajikita kuendeleza wajasiriamali wadogo, wa kati na wakubwa ambayo ni nguvu kazi ya Afrika kiuchumi,” alisema.

Aidha, alisema ni muhimu wanawake na vijana wakajengewa uwezo kupitia elimu na sayansi na teknolojia ili kujenga na kukuza Afrika kiuchumi na kibiashara.

Alitolea mkazo suala la elimu kwa vijana hasa kwenye matumizi ya teknolojia akiitolea mfano nchi ya China ambayo uchumi wake kupitia sayansi na teknolojia unajengwa na vijana kuanzia umri wa miaka 18 hadi 35.

“Natoa wito kwa mkutano huu, utoke na mapendekezo ya kisera na mikakati madhubuti kuimarisha uwezo wa wanawake na vijana kutumia fursa zinazotokana na mkataba wa eneo huru la biashara. Tunapaswa kutumia eneo huru la biashara kama jukwaa la uwezeshaji wa wanawake na vijana Afrika ikiwa ni miongoni mwa ajenda muhimu ya mwaka 2063,” alisema Rais Samia.

Alisema ni muhimu kongamano hilo liwekeze zaidi katika rasilimali watu hasa  wanawake na vijana kwa kuwa kukiwa na nguvu kazi yenye ujuzi wa kutosha rasilimali zilizopo zitatumiwa vizuri na kuziongezea thamani na kuiwezesha Afrika kuwa na ushindani kwenye soko la dunia.

Rais Samia alisema mojawapo ya fursa hizo ni itifaki hiyo kutoa upendeleo wa kipekee kuhakikisha baadhi ya manunuzi makubwa ya umma yanafanywa na kampuni zinazomilikiwa na wanawake na vijana.

“Hapa Tanzania sheria ya manunuzi inasema asilimia 30 ya manunuzi yapewe kwa kampuni zinazomilikiwa na wanawake. Sheria ipo lakini utekelezaji bado si mzuri, najaribu ku push (kusukuma) kwa hilo. Ni vyema msaada utolewe kwa wajasiriamali wadogo ili kukuza kipato chao na uchumi na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Hata hivyo, Rais Samia alitumia fursa hiyo kutaja mambo yanayowakwaza wanawake na biashara katika biashara kuwa ni pamoja na mitaji au mikopo kwa ajili ya kuendesha biashara.

Alilitaka eneo hilo huru na nchi za Afrika kwa ujumla kuondoa vikwazo vya biashara na kuboresha miundombinu ili kuimarisha zaidi mazingira ya biashara Afrika.

Alisema Tanzania imeanza kuondoa ubaguzi wa kijinsia katika biashara na akasema upo unyanyasaji kwa wanawake masokoni.

“Tanzania inafanyia kazi hilo ili kulifanya eneo la soko kuwa eneo la watu wote wanawake na wanaume. Pia tunataka kuchukua hatua ya kutengeneza jamii yenye usawa wa kijinsia,” alisema Rais Samia.

Aidha, alizungumzia umuhimu wa Afrika kuwa na takwimu sahihi ili kuwa na mipango mizuri na kusaidia wananchi wake kiuchumi.

“Tuwe na takwimu sahihi ili tujue tunafanyaje biashara Afrika, nani anafanya biashara na eneo lipi na bidhaa gani, kuuza nje na ndani tunauza nini na wapi takwimu zitatusaidia kwa hili. Pia tutapata picha ya kutambua soko na nini tuzalishe Afrika na nani anahitaji bidhaa gani Afrika,” alisema.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alisema kongamano hilo ni fursa ya kuwakwamua wanawake na vijana kiuchumi kwa kuwashirikisha katika mkataba wa eneo huru la biashara Afrika.

Kongamano hilo, limehudhuriwa na viongozi Afrika akiwemo Rais wa Ethiopia, Sahle Zewde kwa njia ya mtandao, Rais Mstaafu wa Malawi, Dk Joyce Banda na Makamu wa Rais wa Uganda, Jesca Alupo.