Samia: Tanzania ni tajiri wa madini

Samia: Tanzania ni tajiri wa madini

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania ina utajiri wa madini hivyo anataka umakini kuchagua washirika wa kuvuna fursa ya utajiri huo.

Pia, ameagiza wawekezaji waliosaini na kuwekeza katika uchimbaji wa madini wasichelewe kuanza kutekeleza miradi hiyo ili nchi inufaike.

Rais Samia alisema hayo Ikulu Chamwino, Dodoma jana baada ya kushuhudia kusainiwa mikataba ya makubaliano kati ya serikali na kampuni tatu za madini kutoka Perth nchini Australia.

Advertisement

“Tuna mtindo wa kupokea miradi tunachukua fedha tunapeleka kwenye stock exchange (masoko ya hisa na mitaji) tunavuna kwanza fedha halafu ndio uwekezaji uendelee, huu kwetu ni uhujumu uchumi. Twende pamoja moja kwa moja,” alisema na kuongeza:

“Nataka niwathibitishie kutokana na juhudi zilizofanywa na serikali, ukuaji wa sekta ya madini na mchango wake katika pato la taifa umeendelea kuimarika. Nakumbuka mwaka juzi nilipomteua kuwa Waziri wa Madini (Doto Biteko) nikamwambia katika mipango yetu ya maendeleo sekta ya madini inatakiwa ichangie asilimia 10 ifikapo 2025, lakini furaha yangu kabla ya 2025, sekta hii inakaribia kufika asilimia 10.”

Rais Samia alisema katika siku zijazo Tanzania itakuwa kitovu cha uzalishaji na usafishaji wa madini adimu, hivyo kuvutia zaidi uwekezaji.

“Sasa ni madini haya ambayo yanakuza jina la Tanzania duniani na nchi zenye nguvu sasa zinaangalia Tanzania,” alisema Rais Samia na kuongeza:

“Nchi yetu imebarikiwa madini mbalimbali ikiwemo kinywe na mengine ambayo ni nadra kupatikana duniani. Yapo madini ya chuma, dhahabu, nikeli, fedha, shaba, tanzanite, safaya, rubi, chokaa, chumvi, makaa ya mawe, urani na mengineyo yanayopatikana maeneo mbalimbali kulingana na ukanda wa kijiolojia.”

Rais Samia alisema kutokana na tafiti zilizofanywa yapo maeneo ambayo awali yalionekana masikini hayana vyanzo vya fedha lakini kumbe Mwenyezi Mungu ameficha madini ardhini.

Alisema mikoa ya Lindi na Morogoro kwa sasa imebainika kuwa iko kwenye ukanda wa madini ya kinywe wakati Songwe imebainika kuwa na madini adimu.

Rais Samia alisema kwa mujibu wa utafiti uliofanywa mwaka 2000 kuhusu madini ya kinywe na adimu hadi sasa kuna mashapo ya tani milioni 67 zenye wastani wa asilimia 5.4 ya madini ya kinywe yaliyogundulika katika Kijiji cha Chilalo mkoani Lindi ambayo yatachimbwa kwa miaka zaidi ya 18.

Pia, imebainika kuwepo kwa tani milioni 63 zenye wastani wa asilimia 7.6 za madini ya kinywe yaliyogundulika katika Kijiji cha Epanko mkoani Lindi yatakayochimbwa kwa miaka zaidi ya 18 na tani milioni 18 zenye asilimia 4.8 za madini adimu zilizogundulika katika Kijiji cha Ngwala mkoani Songwe yatakayochimbwa kwa muda wa zaidi ya miaka 20.

“Madini haya ya kinywe na adimu yapo kwenye orodha ya madini muhimu ya kimkakati duniani, kutokana na kuhitajika sana katika teknolojia mpya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo hutumika kutengenezea betri za magari ya umeme, vifaa vya kielektroniki na mitambo mbalimbali,” alisema Rais Samia.

Alisema katika ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris nchini hivi karibuni, walizungumzia madini hayo na ya mradi wa madini ya Kabanga na kiwanda cha usafishaji madini kitakachojengwa Kahama.

Rais Samia alisema ili nchi iweze kunufaika na madini hayo serikali iliamua kuingia makubaliano na kampuni zenye uwezo wa kuvuna na kuchakata madini hayo nchini ili Watanzania wanufaike.

“Sasa fursa hizi tulizopewa na Mungu tusichukulie kwa wepesi bali itupe umakini mkubwa katika kuchagua nani tushirikiane naye kuvuna rasilimali hizo…kwa maslahi mapana ya Taifa letu,” alisema.

Rais Samia alisema serikali imekuwa ikifanya mazungumzo na wawekezaji na kukubaliana kuunda kampuni za ubia na mbali na umiliki wa hisa uliowekwa kisheria wa asilimia 16, serikali itanufaika kupitia kodi, tozo, ajira, maendeleo ya miundombinu, ukuaji wa teknolojia, kukuza uwezo wa utaalamu na urejeshaji wa hisani au huduma kwa jamii.

Alisema kutokana na makubaliano hayo na kuwekwa sheria za kusimamia makubaliano hayo ndio maana kumekuwa na mazungumzo ya muda mrefu na wawekezaji hao na kuunda kampuni za ubia ambayo ni Kudu Graphite Ltd, Duma Tanza graphite Ltd, Mamba Mineral Cooperation na Mamba refinery Cooperation.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *