Samia: Tanzania tumejipanga kuwa ghala la chakula Afrika

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania imejipanga kuwa ghala la chakula Afrika na mikakati iliyowekwa ni pamoja na kufufua mashamba yote nchini na kuunda mfuko wa Kuimarisha Kilimo Tanzania (AGTF).

Kauli hiyo ameisema jana Ikulu, Dar es Salaam wakati akizindua Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF).

Akizungumza kabla ya kuzindua jukwaa hilo, Rais Samia alisema sekta ya kilimo kwa sasa huchangia asilimia 25 ya pato la taifa na kuwa serikali imeamua kutoa kipaumbele katika sekta ya kilimo na kuhakikisha nchi inakuwa ghala la chakula Afrika.

Advertisement

“Tumejipanga Tanzania iwe na uhakika wa usalama wa chakula na lishe tuitangazie dunia nchi yetu ni ghala la chakula,” alisema Rais Samia.

Alisema takwimu za sasa kuhusu upatikanaji wa chakula duniani zinaonesha kuwa baada ya janga la virusi vya corona (Covid-19) duniani mtu mmoja kati ya watano ana njaa.

Alisema ili kufikia lengo la kuwa ghala la chakula Afrika, serikali imejipanga kuboresha sekta ya kilimo kwa kutoa pembejeo bora za kilimo kwa wakulima kwa wakati, kuwajengea uwezo vijana na ili watumike kwenye sekta hiyo, kufungua masoko ya kimataifa, kuboresha miundombinu ya kilimo na kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvunwa.

Alisema kwa kufanikisha hilo Machi 20, mwaka huu atazindua mjini Dodoma programu ya mafunzo kwa vijana (BBT) ambayo Wizara ya Kilimo ilitangaza fursa ya mafunzo kwa vijana hivi karibuni na awamu ya kwanza vijana 800 wanakwenda kunufaika.

Akizungumzia kuundwa kwa mfuko wa AGTF nchini ambao utatumika kusaidia sekta ya kilimo na wakulima wote, Rais Samia alisema utakuwa unatoa fedha kwa ajili ya pembejeo za kilimo na pia utatumika kugharamia mafunzo ya vijana wanaoingia katika programu ya BBT ya kilimo.

Aidha, alitoa rai kwa wadau wote katika mnyororo wa sekta ya kilimo kuhudhuria Kongamano la AGRF, litakalofanyika Septemba 5 hadi 8, mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe akizungumza katika uzinduzi huo alisema Tanzania ina jumla ya hekta milioni 44, zinazofaa kwa kilimo na pia ina hekta milioni 29, zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kuwataka wawekezaji waje kuwekeza.

Alisema lengo la nchi ni kujitosheleza kwa chakula na kuuza nje na kusema ardhi ya kilimo nchini ipo ya kutosha na kutaka wawekezaji kuja kuwekeza katika sekta hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa AGRF, Amat Pathe Sene alisema lengo la jukwaa hilo ni kuona Afrika inazalisha chakula cha kutosha na pia vijana wachangamkie  fursa ya kilimo kuinua maisha yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Chakula Afrika (AFP), Dk Jakaya Kikwete akizungumza katika uzinduzi huo alimpongeza Rais Samia kwa kuinua sekta ya kilimo kwa kiwango kikubwa ndani ya muda mfupi.

Kikwete ambaye ni Rais mstaafu aliwataka mawaziri wanaohusika na sekta ya kilimo na mifugo kuchapa kazi zaidi na wasimuangushe Rais.

Alisema jambo kubwa lililofanywa na Rais Samia ni kuwahusisha vijana na wanawake kuingia katika fursa ya kilimo na hiyo itasaidia kuinua nguvu kazi hiyo kubwa kuleta maendeleo nchini.

 

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *