Samia: Tanzania, Zambia zisishindane, ziwezeshane
RAIS Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania na Zambia zisishindane ila ziwezeshane kibiashara ili kujikomboa kiuchumi.
Pia Rais Samia ameunga mkono maagizo ya Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema kwa wafanyabiashara wa nchi hizo kwamba waache kulalamikia serikali, wawasilishe maoni ya namna ya kutumia fursa zilizopo katika nchi hizo mbili.
Alisema hayo jijini Lusaka juzi jioni katika Jukwaa la Biashara la Tanzania na Zambia na akasema nchi hizo zinapaswa kupambana kupata uhuru wa kiuchumi.
Rais Samia alisema Tanzania na Zambia zimejaliwa rasilimali za asili na rasilimaliwatu za kutosha hivyo nchi hizo si masikini ila zinahitaji kushirikiana ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi.
Alihimiza wafanyabiashara waseme wanataka nini kutoka serikalini ili serikali ichukue hatua kukuza biashara baina ya Tanzania na Zambia.
Rais Samia alisema Tanzania ipo tayari kufanya biashara na Zambia na milango iko wazi kukaribisha wawekezaji.
“Naomba kupitia vyama vyenu vya kibiashara na ubalozi wetu hapa Zambia wasilisheni changamoto lakini pia mafanikio mnayoyapata kwa kufanya biashara na Tanzania,” alisema.
Rais Samia alihimiza wafanyabiashara watengeneze mtandao wa kibiashara na wafanye biashara kwa ubia.
“Tunaamini sekta binafsi ndio injini ya uchumi. Networking ni muhimu sana, nawashauri mfanyekazi kwa kushirikiana kurahisisha kazi zenu,” alisema.
Aidha, Rais Samia alisema Tanzania ina utashi wa kisiasa kuongeza kiwango cha biashara baina yake na Zambia hivyo wafanyabiashara waitumie fursa hiyo.
“Tunatengeneza mazingira mazuri ya biashara. Karibuni Tanzania, usipowekeza Tanzania unakosa mengi,” alisema.
Rais Samia alisema Tanzania ina soko kubwa, miundombinu bora lakini pia pato lake la taifa linakua kwa asilimia sita na maendeleo ni mazuri.
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema alisema serikali za nchi zote mbili ziko tayari kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara.
“Tunahitaji ushirikiano zaidi kibiashara. Mje na mawazo ya kibiashara na uwekezaji kulingana na fursa zilizopo katoka nchi zetu. Yatakayoibuliwa yawe wazi yaoneshe mnachotaka,” alisema Rais Hichilema.
Aliongeza: “Msilalamike sana Samia hafanyi hivi HH hafanyi vile hapana. Nyinyi mnataka nini? Hili si suala letu pekee bali pia nyie.”
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji alisema Tanzania na Zambia zinafanya jitihada kuboresha mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na kuondoa vikwazo visivyo vya kikodi.
Alisema hadi sasa kati ya vikwazo 24 vinane vimeondolewa na 16 wamekubaliana ifikapo Desemba, mwaka huu visiwepo.