DODOMA: RAIS Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali itafanyia kazi mambo yaliyoibuliwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na taarifa ya utendaji kazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Rais Samia amesema hayo leo Machi 28, 2024 Ikulu Chamwino jijini Dodoma mara baada ya kupokea ripoti hizo alizokabidhiwa na CAG Charles Kichere na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Salum Hamduni.
Amesema, ripoti hizo zinazosomwa kila mwaka zinachangia kuimarika kwa utendaji ndani ya serikali na mashirika ya umma.
“Kuna dosari zilizotolewa hapa tutaenda kuzifanyia kazi kisawasawa turekebishe na mwakani pengine hizi hazitajirudia tutakuwa tumesogea,” amesema
Pia Rais Samia amesema ripoti hizo zinaonesha kwamba kuna maboresho yaliyofanyika katika masuala ya usimamizi wa fedha za umma, kwani ripoti ya CAG imeonesha hati safi zimeongezeka hadi kufikia asilimia 99, hati zenye shaka tisa, sawa na asilimia 0.7 na hatichafu moja sawa na asilimia 01.