DAR ES SALAAM: Rais Samia Suluhu Hassan amesema Taifa linapaswa kujivunia maono ya Waasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwani kwa sasa ni muda wa kuvuna matunda ya muungano huo.
Rais ametoa kauli hiyo katika Sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano iliyofanyika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam leo Aprili 26, 2024 ambapo amesema ni lazima taifa liendelee kuyaenzi maono ya viongozi hao.
“Kwa niaba yenu Wananchi Watanzania ninawashukuru kwa dhati Waasisi wa Muungano huu Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume pamoja na viongozi waliofuata baada yao kwa kutuleta pamoja na kujenga taifa huru, madhubutu na lenye matumaini” amesema Samia na kuongeza
Zawadi pekee tunayoweza kuwapa ni kuendeleea kudumisha Muungano huu na kuyaenzi maono yao. Kwa msemo wa sikuhizi tunasema tuwape maua yao.”
Marais mbalimbali kutoka Afrika wamehudhuria maadhimisho hayo; Rais wa Kenya William Ruto, Rais wa DRC Felix Tshisekedi, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, Rais wa Umoja wa Comoros Azali Assoumani , Rais wa Jamhuri ya Zambia Hakainde Hichilema, Rais wa Shirikisho la Somalia Hassan Sheikh Mohamud na Rais wa Jamhuri Namibia Nangolo Mbumba.