Samia: Uzazi isiwe huzuni kwa familia

DAR ES SALAAM: RAIS Samia Suluhu Hassan amesema familia zinastahili kufurahi anapozaliwa mtoto badala ya kuhuzunika. Ameeleza hayo kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa X wakati akizungumzia ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Mkumbi wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.

Rais Samia amesema kujengwa kituo hicho ni sehemu ya ujenzi wa vituo 1,324 unaoendelea katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

“Kuzaliwa kwa mtoto inapaswa kuwa tukio la furaha kwa familia na jamii nzima badala ya huzuni hasa pale inapotokea kupoteza mtoto, mama au wote kwa pamoja,” aliandika Rais Samia. Ameongeza,

“tunaendelea kuifanya kazi ya kuboresha huduma zetu za afya ili kukabiliana na changamoto hii ya mwanzo wa maisha ya kila binadamu kwa kuongeza ukaribu wa upatikanaji wa huduma za afya, vifaa, ubora na uwezo wa kukabiliana na dharura”.

Hivi karibuni, Wizara ya Afya ilisema utashi wa kisiasa na uongozi wa Rais Samia kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto umewezesha Tanzania kupunguza vifo vya wajawazito kutoka vifo 556 hadi 104 katika kila vizazi hai 100,000.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema hayo Geneva nchini Uswisi wakati wa mkutano kujadili mikakati ya kupunguza vifo vya wajawazito.

Mkutano uliandaliwa na Umoja wa Afrika (AU), Wizara ya Afya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa Afya ya mama na mtoto ambao ni taasisi za EGPAF na Save the Children. “Tangu akiwa makamu wa rais aliasisi kampeni mahususi ya kupunguza vifo vya wajawazito na watoto sambamba na kuwasainisha mikataba wakuu wa mikoa ili kuwajibika katika maeneo yao katika suala hili,” alisema Ummy.

Aidha, alisema mbinu nyingine zilizotumika hadi kupunguza vifo vya wajawazito kutoka vifo 556 hadi 104 katika kila vizazi hai 100,000 ni kuimarisha ubora wa huduma ikiwamo uwajibikaji katika ngazi za utoaji huduma za afya nchini.

“Hatua nyingine ni kuwapo kwa sharti linalotaka kituo /hospitali yoyote inayopata kifo cha mjamzito kufanya mapitio ya kila kifo cha mjamzito katika vituo vya umma ndani ya masaa 24 na kuweka mpangokazi ili kisitokee kifo kingine,” alisema Ummy.

Alisema pia uwekezaji katika miundombinu ya upasuaji kwa wajawazito, dawa za uzazi salama na uwapo wa mfumo wa rufaa wa dharura kwa wajawazito M-Mama. Pia ushirikishwaji wa vyama vya kitaaluma umefanikisha Tanzania kupata mafanikio makubwa katika kupunguza vifo vya wajawazito.

 

Habari Zifananazo

Back to top button