Samia: Viongozi mjitathmini

Rais Samia

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa Serikali kujitathmini kwa nafasi zao kama wana maadili ya uongozi.

Rais Samia amezungumza hayo alipofanya mkutano wa faragha wa Mawaziri, Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa Arusha (AICC) jijini Arusha leo Machi, 02 2023.

“Watu tunao, ardhi tunayo na siasa safi ipo, suala la kujadili ni kuhusu uongozi bora, baada ya kumaliza kikaokazi hiki kila mmoja ajitathmini kama maadili ya kiongozi bora tuliyoambiwa yapo au laa.” Amesema Rais Samia.

Advertisement

Rais Samia amesema lengo la kikao hicho ni kuelekezana juu ya kutimiza ipasavyo wajibu wa viongozi na dhamana waliyonayo ya kuwatumikia Wananchi.

Rais Samia amesema ukumbusho wa kuzingatia maadili ya uongozi alioutoa kwa viongozi wa serikali hauwalengi viongozi wapya walioteuliwa hivi karibuni. “mkutano huu ni muhimu zaidi kwa viongozi wazoefu.”

“Katika jukumu lenu la utawala, mnategemewa kuwa makini na mahiri katika kutumia na kusimamia rasilimali watu, vifaa na fedha za umma pamoja na kuwa na mipango na mikakati thabiti ya kutekeleza na kusimamia majukumu hayo.” Amesema Rais Samia.

Katika mkutano huo wenye lengo la kuwakumbusha viongozi wa serikali namna bora ya utendaji kazi na kuzingatia maadili,Rais Samia amesema kuwa ili viongozi ahao waweze kutimiza wajibu wao kikamilifu wanapaswa kutambua mpika yao ya kazi.

“Ni wajibu wenu kuzifahamu kwa kina shughuli za wizara zenu ili ziweze kufanyika kwa umakini na uweledi, vinginevyo mtashindwa kupanga malengo kwa walio chini yenu kwani mtakuwa hamjui nini cha kuelekeza na mtashindwa kusimama kwa kuwa hamjui nini cha kusimamia.”