Samia: Viongozi wa dini kemeeni maovu

Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini nchini wakemee maovu zikiwemo na dhuluma, mauaji na mmomonyoko wa maadili.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana aliposhiriki Baraza la Maulid lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW).

Rais Samia aliwashukuru viongozi wa madhehebu ya dini kwa ushirikiano baina yao bila kujali dini zao.

Advertisement

“Suala la maadili nalo nahimiza Bakwata na viongozi wengine wa dini mkalisemee hili, mtetereko umetokea ndani ya taifa letu, kama viongozi,walezi tulitetereka mahali turudi tufundishane, tuelekezane, tushike maadili,”alisema.

Rais Samia alisema wadau wote ni muhimu washirikiane na viongozi wa dini ili kuhakikisha jamii inakuwa na watu waliojengwa kimaadili na kuacha matendo maovu yanayotendeka na kuhuhudiwa katika jamii.

“Tunaomba wadau wote kwenye hili la maadili muungane tuhakikishe jamii inajengwa katika misingi ya maadili, bado dhuluma ipo, viongozi wa dini mkayasemee ili kupunguza hayo katika jamii. Tumuenzi mtume kwa kufuata mafundisho, serikali iko pamoja na nyie,”alisema.

Rais Samia alisema matendo maovu au mema hayaangalii dini, yanafanywa na yoyote hivyo kama taifa linapaswa kuendelea kupendana na kuheshimiana kwa kuhakikisha jamii zina maadili kama mafundisho ya dini zote yanavyosema.

Aidha alitoa rai wa familia kuhakikisha wanajipanga kutumia sayansi na teknolojia na kuwahi nyumbani ili kupata muda wa kukaa na familia kufundishana maadili na nidhamu.

Mufti na Shehe Mkuu wa Tanzania, Abubakar Zuberi alisema jamii isipokuwa na tabia njema  au maadili mema huwa haina mafanikio na matokeo yake taifa lake linaangamia.

“Viongozi wote wa dini tukemee mmomonyoko wa maadili na udhalilishaji wa watoto na tukemee ili umma na watanzania tuende kwenye njia iliyonyooka,”alisema Shehe Zuberi.

Katibu Mkuu wa Bakwata, Jabir Mruma alisema matukio ya uhalifu na vitendo viovu kama mauaji, wizi ni mambo yanayoripotiwa katika jamii na hayakubaliki katika jamii iliyostaarabika.

“Tunalaani matendo hayo na kutaka jamii ibadilike na kufuata matendo mema.Tunatoa mwito wa viongozi katika jamii kuendelea kusisitiza jamii kutenda na kufanya mema na kuchukia maovu, tuendelee kutunza tunu ya amani,”alisema Mruma.

Alisema katika kusherekea Maulid ya Mtume, ni vyema jamii ikafuata mafundisho adhimu yanayoelekeza kutenda mema.

Alisema Bakwata na Baraza la Ulamaa lilitoa tamko na kutaka mtoto wa kike apate haki sawa kama ilivyo kwa mtoto wa kiume ili kukomesha ndoa za utotoni.

Awali Mjumbe wa Baraza la Maulamaa, Shehe Hamid Masoud Jongo alisema kumomonyoka kwa maadili hasa kwa vijana hadi kujipa majina ya ajabu kama panyaroad, inaashiria ndani ya familia hakuna maadili.

“Hili la momonyoko wa maadili hadi vijana kijipa majina ya panya road inabidi tumlete mtume ndani ya nyumba zetu na kujenga maadili ndani ya familia, kwa sababu hao vijana wana majina yetu, sasa hayafanani ya matendo yao,tunawajibu kwenye malezi,”alisema Shehe Masoud.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala alishukuru mshikamano wa Bakwata na wadau wengine wa Kamati ya Amani kwa kuendelea kushirikiana na viongozi wa mkoa kudhibiti vitendo vya uhalifu wakiwemo panyaroad.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *