Samia: Wakristo tumieni Kwaresima kuomba amani

Rais Samia.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewatakia Wakristo wote nchini mfungo mwema wa Kwaresima na kuwasihi kuendelea kuiombea nchi na dunia amani na upendo.

Ameyasema hayo jana kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa Twitter.

Rais Samia alisema katika hija hiyo ya kiroho iliyoanza jana kwa Ibada ya Jumatano ya Majivu, iwakumbushe Wakristo kuhusu ubinadamu wao na kumrudia Mwenyezi Mungu huku wakiomba ulinzi wake kwa watu wote.

Advertisement

“Nawatakia Kwaresima njema Wakristo wote. Katika hija hii ya kiroho mnayoianza leo kwa Jumatano ya Majivu, endeleeni kuiombea nchi yetu na Dunia nzima amani na upendo. Majivu katika paji la uso yawakumbushe ubinadamu wenu na kumrudia Mwenyezi Mungu, mkiomba ulinzi wake kwetu sote,” aliandika Rais Samia.

Kwaresima ni kipindi cha toba kwa siku 40 kutafakari zaidi mateso ya Kristo aliye kielelezo na chimbuko la ukristo. Jana gazeti hili liliripoti ujumbe wa mwaka huu wa Kwaresima wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (T.E.C) unaosema: “Tunawaombea Mjaliwe Kufanywa Imara Katika Utu…” unaotoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Waefeso 3:16.

Katika ujumbe huo wa TEC, pamoja na mambo mengine, ulisisitiza wazazi kuwafundisha watoto wao kukua katika mapendo na imani wakiwa katika umri mdogo ili kujenga taifa la baadaye lenye kuheshimu utu wa binadamu.