Sanaa kuboresha maslahi ya wasanii Iringa

OFISA Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania, Nyakaho Mahemba amewataka wasanii wa fani mbalimbali mkoani Iringa kujiandaa kunufaika na mfuko huo kwa kuandaa sanaa zitakazoboresha maslai yao na kukuza uchumi wao.

Kwa kupitia benki za NBC na CRDB, mfuko huo unatarajia kutoa mikopo mipya ya zaidi ya Sh bilioni 20 kwa wasanii mbalimbali hapa nchini kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024.

Advertisement

Mahemba aliyasema hayo mjini Iringa kwenye  semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wasanii mbalimbali wa Mkoa wa Iringa juu ya namna wanavyoweza kunufaika na mikopo hiyo.

“Serikali ya awamu ya sita kupitia Mfuko wa Sanaa imeamua kutatua changamoto ya wasanii ambayo ni mtaji kwa kuwapatia fursa ya mikopo na elimu ya namna itakayowawezesha kuboresha kazi zao ili mikopo watakayopata iwape tija,” alisema.

Alisema mfuko huo unatoa huduma katika maeneo ya urithi wa utamaduni, lugha na fasihi, sanaa za maonesho, sanaa za ufundi, filamu, muziki na fani nyingine zenye mlengo wa utamaduni na sanaa kwa watu binafsi, vikundi au makundi.

Alisema tangu uzinduliwe Disemba mwaka jana,  mfuko huo tayari umekwishatoa mikopo yenye thamani ya Sh bilioni 1.077 kwa wadau wa tasnia 45 ambao kati ya wanaume ni 29waliowezeshwa Sh milioni 737, wanawake 12 Sh milioni 275, kikundi kimoja Sh milioni 10 na makampumi matatu Sh milioni 55.

“Miongoni mwa wanufaika hawa ni kundi la walemavu lenye wanachama 22 wanaojishughulisha na uandaaji wa tamthilia, uibuaji wa vipaji vya tasnia kwa walemavu wenzao na watoto,” alisema.

Meneja wa Bidhaa na Huduma wa makao makuu ya benki ya NBC, Dar es salaam Jonathan Bitababaje alisema benki yao inayofuruaha na inatarajia mafanikio makubwa kwa kuingia ushirikiano na serikali ili kufanikisha mpango huo wa utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa wasanii.

“Mikopo inayotolewa inaanzia Sh 200,000 hadi Sh milioni 100 kwa mkopaji mmoja. Tunawaomba wasanii wa Iringa nendeni katika ofisi za utamaduni katika wilaya zenu na mkoa ili mkajiandikishe na kuanza taratibu za kunufaika na mikopo hii,” alisema Bitababaje.

Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Viwanda na Bishara, Asifiwe Mwakibete amewataka wasanii wa mkoa huo kuichangamkia fursa hiyo na kuhakikisha wanatumia fedha za mfuko huo kuinua sanaa na kazi zao kwa ujumla.

Akiwataka waongeze ubunifu ili kujiweka katika mazingira ya kupata soko la uhakika, Mwakibete amewataka wasanii watakaonufaika na mpango huo kuwa waaminifu katika urejeshaji wa mikopo hiyo ili iweze kuwasaidia na wengine.

Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji Mkoa wa Iringa Hamis Nurdin ameishukuru serikali kwa kuwaletea fursa hiyo akisema watahakikisha wanaitumia ipasavyo ili isaidie kuboresha kazi zao na hatimaye kuwaingiza katika soko la ushindani.

7 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *