UMOJA wa Waganga wa Tiba Asili Wilaya ya Hitilima mkoani Simiyu, wamemsimika jina la Masanja Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana.
Akizungumza leo Julai 28,2023 Katibu wa Waganga wa Tiba Asilia Wilaya ya Hitilima, Japhary Sitta amesema wamempa jina hilo kutokana na uwezo wake, umakini na ubunifu alionao wa kushawishi na kukusanya makundi mbalimbali ya watu, kwa lengo la kuleta mshikamano ndani ya CCM na nje ya chama hicho.
“Tunakupatia jina hili la Kisukuma kuanzia sasa utaitwa Masanja, kwa heshima na taadhima tunakuomba upokee jina hili la Masanja lenye maana ya upatanishi wa makundi mbalimbali, ” amesema Katibu wa sangoma hao..
Amesema, jina hilo litaenda sambamba na kazi aliyopewa na Chifu Hangaya Rais Samia Suluhu Hassan kusimamia maridhiano ya vyama siasa nchini.
“Sisi waganga wa asili wa Hitilima, tupo 2, 876, tutaendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwenye Chama Cha Mapinduzi na serikali yake, ” amesema na kukemea vitendo vya baadhi wa Watanzania wanaobeza Muungano.
” Tunakemea vikali wale wote wanaopinga jitihada za Rais Samia kuleta maendeleo ya taifa letu,” amesema.
Kwa upande wa Kinana amesema amefurahishwa na jina hilo hasa baada ya kuelezwa maana yake kuwa ni upatanishi na kiunganishi cha makundi mbalimbali.
“Sijisifu lakini katika kipindi chote cha maisha yangu nimejitaidi kupatanisha watu mbalimbali na makundi mbalimbali, kuanzia sasa mimi ni familia ya kina Masanja, familia kwa maana ya kuyatenda yote yanayoendana na jina hili.
“Kuanzia sasa mkiwa na shughuli yoyote kubwa mkinialika nitakuja,” amesema.
Comments are closed.