Saratani ya homa ya ini tishio nchini
KATI ya watu 684 waliopimwa saratani ya homa ya ini kwa siku mbili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) mkoani Dar es Salaam, watu 30 wamebainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Kutokana na idadi hiyo, wataalamu wa afya nchini wameshauriwa kuunganisha nguvu kuzuia magonjwa ya saratani hususani saratani ya ini kwa kuipa jamii uelewa kuhusu dalili, njia za maambukizi na matibabu kwa kuwa jamii haina uelewa wa kutosha kuhusu ugonjwa huo.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Rashid Mfaume kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Serikali alipofungua Kongamano la Kwanza la Saratani ya Ini linalofanyika kwa siku mbili kuanzia Machi 17 hadi 18, mkoani Dar es Salaam.
Dk Mfaume aliongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa takribani watu milioni 91 Afrika wanaishi na saratani za aina mbalimbali za ini.
Aidha, alisema wengine wanakabiliwa na ugonjwa huo katika umri mdogo jambo ambalo sio la kawaida kwa nchi zilizoendelea.
“Tumeona kuwa kuna haja ya kufanya tafiti kujua ukubwa wa tatizo la saratani ya ini nchini, tumeshauriana tafiti zifanyike maeneo ya vijijini na mijini kwa kuwa inawezekana visababishi na viashiria vinatofautiana,” alisema Dk Mfaume.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi alisema Muhimbili inatambua umuhimu wa kuunganisha nguvu kukabiliana na magonjwa aina mbalimbali, ndio maana ilitoa ushirikiano katika maandalizi ya kongamano hilo.
Profesa Janabi alisema matibabu ya saratani ya ini yana gharama kubwa, ambako ni takribani Sh milioni 30 kwa mgonjwa mmoja hivyo ni vyema kujikinga kutopata saratani hii kabla ya kupata maradhi haya.
Naye Mwenyekiti wa kongamano hilo, Dk Ally Mwanga alisema lengo ni kujadiliana namna ya kuunganisha nguvu dhidi ya mapambano ya saratani ya ini nchini ili kuipunguzia serikali mzigo wa matibabu wa saratani hiyo.