‘Saratani ya utumbo, koo zinakuja kasi’

MGANGA Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kazi ulimwenguni na kwamba Tanzania ni moja ya nchi zenye ongezeko hilo, huku ikiorodhesha visa vipya 40,000 vya saratani mwaka mmoja uliopita.

Aidha, amesema Tanzania kama taifa inapaswa kuchukua hatua za haraka kujikinga dhidi ya saratani ya koo na saratani za utumbo mpana zinazokuja kwa kasi.

Alibainisha hayo katika maadhimisho ya Siku ya Mashujaa wa Saratani Duniani katika viwanja vya Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dar es Salaam chini ya taasisi ya Shujaa Cancer Foundation kwa ushirikiano na ORCI.

“Saratani ya kizazi na ya matiti, zinachangia asilimia 35 ya saratani zote nchini, pia kuna saratani ya tezi dume, hii inachangia asilimia 8.8,” alisema.

Akaongeza: “Huu ni mzigo mkubwa kwa taifa kwani matibabu yake ni ghali na ya muda mrefu, hapa pia saratani ya koo na ya utumbo mpana zinakuja kwa kasi. Kama taifa lazima tuchukue hatua za haraka kujikinga.”

Alisema miongoni mwa njia za kuepuka saratani kuwa ni pamoja na kufanya mazoezi kwa nusu saa walau mara nne kwa wiki, kupima afya mara kwa mara, kuepuka vyakula vilivyosindikwa, kuepuka matumizi ya sigara na pombe kupita kiasi.

Alimwagiza Kaimu Mkurugenzi wa Tiba, Wizara ya Afya, kuhakikisha hospitali zote zenye mashine za CT Scanner zinaunganishwa ili zitoe tiba mtandao kwenye kipindi cha miezi miwili ijayo.

Kwa mujibu wa Profesa Nagu, mashine za CT Scan zipo katika mikoa yote Tanzania na kwamba asilimia 98 zinafanya kazi.

“Leo ni tarehe 4 Juni (juzi), ifikapo Agosti 4, hospitali zote ziwe zinatoa huduma ya tiba mtandao. CT Scan tuliyoifunga Rukwa iwe na mawasiliano na Ocean Road, nayo Muhimbili iweze kuwasiliana na Ocean Road, iweze kuwasiliana na Mbeya nakadhalika,” alisema.

Mkurugenzi wa Shujaa Caner Foundation, Glory Kida alisema Siku ya Mashujaa wa Saratani Duniani huadhimishwa kila Jumapili ya Kwanza ya Mwezi Juni ya kila mwaka na kwamba taasisi yake imelenga kuainisha changamoto zinazowakabili wagonjwa wa saratani nchini na kuwasaidia kuishi vizuri.

“Takwimu za kidunia zinaonyesha kwa mwaka 2022 watu milioni 19.3 walibainika kuwa na saratani, hapa Tanzania ni takribani watu 42,000 walibainika. Sisi tumejikita kuwa sauti ya mashujaa wa saratani, tunawaleta pamoja wajue changamoto za saratani, lakini pia namna ya kuishi vizuri na changamoto hizo, tunatarajia kuwafikia wagonjwa 200 ndani ya mwaka mmoja,” alisema Glory.

Habari Zifananazo

Back to top button