Saratani ya utumbo mpana, haja kubwa tishio kwa jamii

Watoto 75 wakutwa na saratani

SARATANI ya utumbo mpana ni matokeo ya viotea au uvimbe ambao awali mtu huishi nao kama viotea vya kawaida na hatimaye hubadilika baada ya kukumbana na visababishi hatarishi.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Saratani, Hellen Makwani anasema ni saratani ambayo huanzia kwenye utumbo mpana na kazi ya utumbo mpana ni kukusanya mabaki ya chakula baada ya mwili kuchukua virutubisho vyote kupitia utumbo mwembamba. “Hufyonza maji katika mwili na kubakiza mabaki ambayo hutoka kama kinyesi,” anasema.

SABABU ZA SARATANI

Advertisement

Anasema saratani ya utumbo mpana husababishwa na baadhi ya vyakula kama nyama nyekundu iliyokaushwa kwa moshi au yenye mafuta sana, kutokula mbogamboga na matunda ambavyo huwa na nyuzinyuzi zinazosaidia mfumo wa chakula kutotuamisha mabaki kwa muda mrefu na kuleta choo kigumu.

Visababishi vingine kwa mujibu wa Dk Makwani ni unywaji wa pombe wa kupindukia, uvutaji sigara, unene kupindukia, kutofanya mazoezi, umri ambapo awali ilikuwa ni miaka 50.

“Lakini kwa sasa tunapata vijana hata wa miaka 20,” anasema.

Anasema kisababishi kingine ni mabadiliko ya kimaisha ambayo hufanya jamii kutumia vyakula vilivyosindikwa au kuhifadhiwa kwenye kemikali mbalimbali na maambukizi ya bakteria aina ya Streptococcus bovis.

DALILI ZAKE

Dk Makwani anasema dalili za saratani ya utumbo mpana ni mtu kutoa choo kigumu na chenye maumivu makali, choo chenye damu, chembamba kikiashiria uvimbe ambao unakuwa ndani ya utumbo na kupunguza kipenyo kuwa kama utepe.

“Dalili zingine ni kukosa hamu ya kula, upungufu wa damu, kupungua uzito, kutapika iwapo kitaziba kabisa na kuharishakutegemeana na eneo la tumbo lililoathirika,” anasema.

VIPIMO VYAKE

Anasema ugonjwa hupimwa kwa ultrasound kuona ukubwa wa tatizo ili kubaini viungo vilivyoathirika, CT scan, X-ray ambayo inaweza kutumika kuangalia kama mapafu yameathirika.

Anasema kipimo kingine ni Colonoscopy ambacho hutumika kumulika sehemu yenye tatizo na kuchukua kinyama kwa ajili ya uthibitisho wa uvimbe na kutoa kinyama kwa ajili ya kupima ili kubaini aina ya seli za saratani.

“Kipimo kingine ni cha damu kwa ajili ya kuangalia kemikali ambayo hutengenezwa na aina hii ya saratani, yaani CEA, ufanisi wa figo, ini na wingi wa damu,” anaeleza.

MATIBABU YAKE

Anasema matibabu ya saratani ya utumbo hufanywa kwa upasuaji ili kutoa sehemu iliyoathirika, kwa tibadawa baada ya upasuaji au kabla iwapo daktari ataona uvimbe ni mkubwa na akipenda usinyae kabla ya upasuaji.

JINSI YA KUJIKINGA

Dk Makwani anasema ili mtu ajikinge na saratani ya utumbo mpana inabidi abadili mfumo wa maisha kwa kupunguza kula vyakula vilivyosindikwa na vyenye mafuta hasa nyama nyekundu. Ufanyaji wa mazoezi ili kupunguza uzito, kula mbogamboga na matunda, kuacha utumiaji wa pombe na sigara, kupunguza ulaji wa nyama nyekundu mfano wa ng’ombe na mbuzi.

NJIA YA HAJA KUBWA

Anasema saratani ya njia ya haja kubwa kwa miaka ya hivi karibuni, imeongezeka. “Wanaume na wanawake wote wanaweza kupata maradhi haya,” anasema Dk Makwani.

Anasema visababishi vya saratani hiyo ni kirusi aina ya HPV ambaye husambazwa kwa kujamiiana kinyume na maumbile, kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ambavyo hushusha kinga ya mwili na kusababisha magonjwa nyemelezi, kuwepo kwa viotea katika njia ya haja kubwa.

Visababishi vingine kwa mujibu wa Dk Makwani ni kuwepo kwa maambukizi ya magonjwa ya zinaa ambayo husababishwa na ngono zembe.

“Kuweka ugoro kwenye haja kubwa kwa wanawake ili kupunguza hisia ya tendo la ndoa,” anasema.

DALILI ZAKE

Anasema mtu hupata maumivu ya haja kubwa hasa wakati wa kujisaidia, muwasho wa njia ya haja kubwa, damu wakati wa haja kubwa au mtu kukuta nguo za ndani zimetapakaa damu, uvimbe kwenye njia ya haja kubwa ambao mtu hufikiri na kutibiwa kama bawasiri.

“Dalili nyingine ni kutokwa kwa majimaji ama ute sehemu ya haja kubwa wenye harufu kali,” anasema na kuzitaja dalili zingine kuwa ni choo kuwa chembamba kama utepe kutokana na ufinyu wa eneo la kutolea.

Visababishi vingine kwa mujibu wa Dk Makwani ni pamoja na upungufu wa damu, kupata mitoki kwenye maungio ya nyonga, kuumwa na nyonga.

Anasema kwa wanawake uvimbe unapokuwa mkubwa hupata maumivu ukeni na mara nyingine hupata fistula ambayo hufanya haja kubwa itokee ukeni.

VIPIMO VYAKE

Anasema vipimo huhusisha kutolewa kinyama kuthibitisha kama ni saratani au la, ultrasound, MRI, CT scan ya tumbo kuangalia iwapo ugonjwa umesambaa na kuathiri viungo vingine mwilini.

“Vipimo vingine ni damu ili kuangalia wingi wa damu pamoja na ufanisi wa figo na ini,” anasema.

MATIBABU YAKE

Dk Makwani anasema matibabu hayo hufanyika kwa mtu kufanyiwa upasuaji iwapo uvimbe ni mkubwa hadi kuziba kabisa njia ya haja. Anasema mhusika hutengeneza njia mbadala ya kutoa choo ambayo kulingana na ukubwa wa tatizo inaweza kuwa ya kudumu au mtu kurejeshewa njia ya kawaida baada ya kupata matibabu.

Anasema matibabu mengine ni ya kutumia tiba ya mionzi ambayo husaidia iwapo tatizo halijahusisha misuli ya kuzuia au kuruhusu choo na kwamba matibabu hayo humuwezesha mtu kuendelea kutumia njia yake ya haja kama kawaida.

Dk Makwani anasema matibabu mengine ni ya tibadawa ambayo hupatiwa iwapo tatizo limehusisha viungo vingine ili kuhakikisha ugonjwa hauzidi kusambaa.

Anasema na kuongeza kuwa tiba nyingine ni tiba shufaa kwa mgonjwa ambaye tatizo lake limefika hatua ya tatu au nne. Anasema tiba hiyo humsaidia mgonjwa kupunguza dalili zote kama maumivu na pia ushauri nasaha kwa mgonjwa pamoja na ndugu wakati wa kipindi chote cha kuuguza.

Anasema vijana wengi hufanya mapenzi ya kuingiliana kinyume na maumbile na imekuwa tatizo kwa watoto wa kike na wa kiume.

“Wazazi tuna jukumu la kusimamia maadili ili watoto wetu wasiige tamaduni za kigeni na zisizofaa,” anasema na kuongeza elimu ya saratani inahitajika zaidi kwa jamii na watu wajenge na kupima afya zao mara kwa mara.

MAONI YA WADAU

Abdallah Maiko mkazi wa Ilemela anasema elimu bado inahitajika kwa wananchi ili waweze kufahamu aina zote za saratani, akisisitiza kuwa serikali iweke mazingira ya kuiwezesha jamii kupata mafunzo kwa awamu kupitia vikao vilivyopo ngazi ya jamii.