‘Saratani yaua 27,000 kila mwaka nchini’

DAR ES SALAAM: KATI ya Watanzania 40,000 wanaogundulika kuugua saratani 27,000 hupoteza maisha kila mwaka huku viashiria vikionesha vifo hivyo huwenda vikaongezeka mara mbili iwapo hatua stahiki hazitachukuliwa ifikapo mwaka 2030.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa takwimu hizo hii leo jijini Dar es Salaam kwenye uzinduzi wa kituo cha huduma za saratani chini ya Hospitali ya Aga khan.

Uzinduzi wa Kituo cha Matibabu ya Saratani cha Aga Khan, jijini Dar es Salaam.

Amesema saratani inayoongoza ni ya mlango wa kizazi kwa asilimia 23.5 hali inayoifanya Serikali kuchukua hatua za makusudi ikiwemo kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupambana na ugonjwa huo unaochangia kupotea kwa nguvukazi za taifa.

https://habarileo.co.tz/vituo-huduma-ya-saratani-kwa-mionzi-kuongezwa/

Naye, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati, Dk Doto Biteko akizungumza katika uzinduzi wa kituo hicho amesema  serikali imejidhatiti kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta mbalimbali nchini ili kuboresha huduma za kijamii ikiwemo afya  ili kuongeza weledi na kuboresha utoaji wa huduma hizo hali itakayosaidia kuongeza kasi ya maendeleo endelevu ya taifa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa nishati, Dk Doto Biteko

“Serikali imejipanga  kuboresha huduma za afya na kupambana na  magonjwa  yasiyoambukiza, tayari serikali imetenga eneo kilipojengwa kituo hiki ambacho kimepanga kuhudumia  wagonjwa 100 kwa siku kwa matibabu ya mionzi, wagonjwa 25 kwa siku kwa tiba za kemikali  na wagonjwa 25 kwa siku kwa uchunguzi wa saratani  na huduma za chanjo,” amesema Biteko.

Aidha, Biteko amesema mradi huo wenye thamani ya jumla ya Euro milioni 13.3 sawa na Sh bilioni 35 umekuwa na mafanikio mbalimbali ndani ya miaka minne ya utekelezaji wake ikiwemo kutoa mafunzo kwa wahudumu 464 na watumishi 400 ngazi ya jamii kuhusu huduma za saratani.

“Kupitia mradi huo wanajamii zaidi ya milioni 4.5 wamepewa elimu kuhusu saratani, watu takriban 700,000 wamepimwa saratani na zaidi ya wagonjwa wapya 39,093 kugunduliwa kuwa na saratani kupitia vipimo stahiki na hivyo kuwawezesha  kuanza kupata tiba stahiki, nawapongeza sana,”amesema.

Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo Mkurugenzi wa tiba kutoka Hospitali ya Aga khan, Dk Harison Chuwa amesema kituo hicho kilichogharimu takribani Sh Bilioni 29.9 chenye vifaa tiba na mashine za mionzi kinauwezo wa kugharamia wagonjwa 100 kwa pamoja na kitasaidia  kupunguza rufaa za wagonjwa wanaoenda nje ya nchi kwa matibabu.

Habari Zifananazo

Back to top button